Volkswagen yazindua kiwanda Kenya
21 Desemba 2016"Baada ya zaidi ya miaka 60 ya kuunda magari ya Volkswagen kwenye mataifa ya kaskazini na kusini mwa Afrika, leo nafurahi kwamba tumepiga hatua hii ya maendeleo nchini Kenya," alisema Dk. Diess wakati wa ufunguzi wa kiwanda hicho nje kidogo ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Rais Kenyatta ameuita uzinduzi huu kuwa ni "ndoto iliyokuwa kweli", akisema kwamba ni ushahidi wa mashirikiano kati ya serikali yake na sekta ya viwanda na hatua kuwa ya kuielekeza Kenya kwenye kuwa taifa la kiviwanda.
Kenyatta ameipongeza serikali ya Ujerumani, Kampuni ya Volkswagen Group na wawekezaji kutoka Ujerumani ambao wameahidi sio tu kutoa mafunzo kwa wafanyakazi katika Kiwanda cha Kuunda Magari cha Kenya Vehicle Manufacturers, bali pia kuijengea uwezo sekta nzima ya uundaji magari.
Gari la kwanza aina ya Volswagen Vivo limeshuhudiwa kukamilika kuundwa katika kiwanda hicho. Diess amempongeza Rais Kenyatta kwa kujitolea kwake kuhakikisha mradi huo umefaulu.
"Ningependa kumshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kusimama na mradi huu. Kuanzia mkutano wetu mjini Berlin hadi kutiwa saini kwa mwafaka wa makubaliano wewe Mheshimiwa Rais ulionyesha kujitolea kwako kwa kujiandaa kufanya mikutano ya mara kwa mara licha ya shughuli zako nyingi."
Rais Kenyatta ameahidi kwamba serikali kuu na serikali za kaunti zitanunua magari kutoka kiwanda hicho kipya ili kuimarisha biashara.
Kampuni ya Volkswagen itaanzisha tena utengenezaji wa magari nchini Kenya ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na inatarajia kuuza magari zaidi katika mataifa ya Afrika Mashariki.
"Baada ya kusitisha kwa muda wa miongo minne uzalishaji wa magari nchini Kenya, Volkswagen itatengeneza magari modeli ya Vivo", walisema Rais Kenyatta na mkuu Volkswagen nchini Afrika Kusini, Thomas Schaefer.
Kampuni ya magari ya Volkswagen inashirikiana na kampuni ya DT Dobbie inayouza na kutengeneza magari ya aina ya Volkswagen nchini Kenya.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef