Von der Leyen atoa wito wa Umoja kati ya Ulaya na AU
7 Desemba 2019
Mji huo ni makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU).
"Ni umoja tu ndio utaweza kufanya mabara yetu kuwa yenye nguvu katika kubadilisha dunia. Umoja wa Afrika ni mshirika namba moja ambae naweza kumtegemea," von der Leyen amesema wakati wa ziara yake nje ya bara la Ulaya kama kiongozi mkuu wa halmashauri tendaji ya Umoja wa Ulaya.
Amesema hatawasilisha "mpango mkubwa kwa Afrika," lakini yuko nchini Ethiopia "kusikiliza" jinsi hali inavyokwenda na maendeleo yanayolijenga bara hilo, pamoja na malengo yake katika siasa na uchumi.
Von der Leyen alianza ziara yake kwa mkutano pamoja na mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki pamoja na makamishina wengine. Pia amepangiwa kukutana na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye hivi karibuni alipata tuzo ya amani ya Nobel, na rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde.
Von der Leyen ameelezea kuhusu ushirikiano wa kimkakati na Afrika kuwa moja katika malengo yake makuu ya masuala ya kigeni, akilielezea bara hilo kuwa ni "jirani yao wa karibu na mshirika wake wa asili."
Halmashauri anayoiongoza von der Leyen itahitaji kufanyakazi na matifa ya Afrika kutimiza lengo muhimu la sera ya kushughulikia uhamiaji, suala linaloleta utata miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Sehemu kubwa ya wahamiaji ambao wanawasili katika mataifa ya Umoja wa Ulaya bila utaratibu maalum wanatoka mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, kwa mujibu wa data za umoja huo.
Moja kati ya mikakati mipya ya halmashauri hiyo kuzuwia uhamiaji ni kuimarisha hali za watu katika mataifa wanayotoka kwa kufanya uwekezaji wa kikanda. Mkakati mwingine ni kuimarisha mpaka wa Umoja wa Ulaya na shirika la ulinzi wa pwani la Frontex.