1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Viongozi wa Ulaya wahimizwa kushikamana kuikabili China

18 Aprili 2023

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amewarai viongozi wa kanda hiyo kuonesha mshikamano linapokuja suala la mahusiano na China.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen Picha: Andy Wong/AP Photo/picture alliance

Kiongozi huyo wa juu wa moja wa Ulaya ametoa mwito huo alipokuwa akitoa hotuba mbele ya wabunge wa Umoja wa Ulaya mjini Strasbourg waliokuwa na mjadala maalumu juu ya mahusiano ya kanda hiyo na China.

Hotuba yake inajiri ikiwa ni wiki moja tangu rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kutoa matamshi yaliyozusha mjadala mkali juu ya ushirikiano kati ya Ulaya na Beijing.

Bibi Von der Leyen amewaambia wabunge hao kwamba sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu China inahitaji umoja na uratibu usioyumba kati ya nchi wanachama na taasisi za Umoja wa Ulaya pamoja na dhamira ya dhati ya kuepusha migawanyiko.

Amezungumzia pia kitisho cha Beijing kutumia mbinu ya kuwagawa viongozi wa kanda hiyo akisema mifano imeoneka katika siku na wiki za karibuni na kuwakumbusha wanasiasa wa Ulaya kuwa muda umewadia wa kuonesha mshikamano usioyumba.

Bila shaka afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya alikuwa akizungumzia kizungumkuti kilichotokea siku chache zilizopita baada ya ziara yake mjini Beijing akiwa pamoja na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Rais Macron alikaririwa akitaka kanda ya Ulaya kutofuata sera ya Marekani kuhusu hadhi ya kiswa cha Taiwan na kujiepusha na kile alikitaja kuwa "mizozo isiyoihusu Ulaya". Mamtashi yake yalizusha ukosoaji mkubwa kutoka kila pembe barani Ulaya.

Von der Leyen agusia umuhimu wa kuendeleza uhusiano na China 

Kutoka kushoto, rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Xi Jinping wa China na rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen mjini Beijing.Picha: Ludovic Marin/Pool AFP/AP/dpa/picture alliance

Ingawa hotuba ya von der Leyen ilijikita kuhimiza mshikamano katika kuikabili China lakini hakupuuza ukweli kwamba pande hizo mbili zinahitajiana.

"Hoja niliyoitoa nikiwa mjini Beijing ni kwamba hatutaki kusitisha uhusiano wetu wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kisayansi na (China). Tuna mafungamano imara na China ni mshirika wetu muhimu kibiashara. Biashara yetu inafikia kiasi Euro bilioni 2.3 kwa siku. Sehemu kubwa ya biashara yetu ya bidhaa na huduma imebakia kuwa yenye manufaa kwa pande zote. Lakini bado kuna ulazima wa kurekebisha mahusiano yetu chini ya misingi ya uwazi, uthabiti na kila upande kuwa na dhamira njema", amesema kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya.

Kupitia hotuba ya leo Von der Leyen aligusia pia umuhimu wa kanda ya Umoja wa Ulaya kupunguza utegemezi wake kwa China katika wakati Beijing inaimarisha nguvu na uwezo wake wa kudhibiti wa bidhaa muhimu za uazalishaji viwandani na teknolojia duniani.

Ama kuhusu suala la Taiwan, Von der Leyen amesema sera ya Umoja huo haijabadilika nayo ni kuheshimu msingi unaotambulika kimataifa wa "China Moja".

Amesema lakini msimamo huo unakwenda sambamba na kuwepo amani na uthabiti kwenye ujia wa bahari wa Taiwan na kwamba Ulaya haitakubali hilo kutetereshwa kwa njia za kutumiwa mabavu.

Katika miezi ya karibuni, mbali ya mahusiano ya kibiashara na mzozo kuhusu Taiwan,  viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakishughulishwa na ukaribu unaongezeka kati ya China na Urusi. Wengi wamefanya ziara mjini Beijing kumsihi rais Xi Jinping kutumia usuhuba wake na rais Vladmir Putin amalize vita nchini Ukraine.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW