1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiCameroon

Wanawake wa Cameroon washinda Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika

1 Desemba 2023

Vuguvugu la kwanza la mashirika na mitandao 77 ya wanawake la Cameroon ndilo mshindi wa Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika kwa kuchangia katika mazungumzo ya amani ya kumaliza mzozo Cameroon

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akitoa hotuba wakati wa Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika mjini Berlin mnamo mwaka 2022
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akitoa hotuba wakati wa Tuzo ya Ujerumani kwa AfrikaPicha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Naibu spika wa bunge la Ujerumani Katrin Göring-Eckardt amesifu kazi ambayo imekuwa ikifanywa na vuguvugu hilo la wanawake tangu kuanza kwa mgogoro nchini Cameroon. Wakati alipokuwa akiwakabidhi wanawake hao tuzo hiyo katika hafla iliyoandaliwa jana mjini Berlin, Göring-Eckardt amesema kuwa zawadi hiyo ni utambuzi wa kujitolea kwao katika kuendeleza amani nchini mwao.

Göring-Eckardt pia aliwapongeza wanawake hao kwa ukakamavu wao licha ya mgogoro nchini humo na hali ngumu walizozivumilia.

Soma pia:Wanasayansi wawili wa Afrika watunukiwa Tuzo ya Ujerumani

Katika mahojiano na DW, katibu wa wakfu huo wa Ujerumani kwa Afrika Sabine Odhiambo, amesema baraza la majaji liliamua kutoa Tuzo hiyo ya Ujerumani kwa Afrika mwaka huu kwa vuguvugu hilo la wanawake kwa mchango wake mkubwa katika utatuzi wa migogoro katika majimbo manne tofauti nchini Cameroon.

Washindi wa Tuzo ya ujerumani kwa Afrika ya mwaka 2023 waahidi kuwahamasisha zaidi wanawake

Katika hotuba ya kukubali tuzo hiyo, wapokeaji wa tuzo hiyo ya mwaka huu wa 2023, waliapa kushughulikia masuala ya utawala yanayoathiri jamii zao. Waliahidi kuwahimiza wasichana na wanawake zaidi kutoangazia jinsia yao kama kikwazo lakini badala yake kama kitu ambacho kinapaswa kuwawezesha kutumikia jamii zao.

Waliopokea tuzo hiyo ni pamoja na Sally Mboumien, mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa shirika la Hatua ya Pamoja kwa Maendeleo ya Jinsia (COMAGEND), linalofanya kazi kuhakikisha haki ya afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na mshindi wa Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika Sikhulile MoyoPicha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Esther Omam, ambaye amefanya kazi katika ushirikiano wa maendeleo na misaada ya kibinadamu nchini Cameroon kwa zaidi ya miaka 20 na Marthe Wandou aliyejitolea kupigania haki za wanawake na watoto kwa zaidi ya miaka 30 ambaye pia ni mmoja wa washindi wa Tuzo ya Haki ya Kuishi ya mwaka  2021.

Mboumien ameiambia DW kwamba kazi za wanawake kwa kawaida ni ngumu kwasababu ya masuala mbalimbali wanayohusika nayo. Mboumien ameongeza kwamba tuzo hiyo ni utambuzi wa juhudi zilizowekwa na wanawake wa Cameroon katika kushughulikia mizozo mbalimbali katika jamii.

Washindi wa awali wa Tuzo ya Ujerumani kwa Afrika

Washindi wa awali wa tuzo hiyo ni pamoja na Sikhulile Moyo na Tulio de Oliveira, wanasayansi wawili kutoka Afrika Kusini waliogundua kirusi cha UVIKO 19 aina ya Omicron. Daniel Bekele, mkuu wa tume ya haki za binadamu ya Ethiopia alishinda tuzo hiyo mnamo mwaka 2021 kwa kutetea haki za binadamu wakati wa kilele cha mapigano kati ya vikosi vya Ethiopia vilivyoungwa mkono na wanajeshi wa Eritrea na kundi la ukombozi wa watu wa Tigray TPLF.

Mnamo mwaka 2020, mwanaharakati wa amani Ilwad Elman mwenye uraia pacha wa Somalia na Canada, alishinda tuzo hiyo kwa mradi wake wa kuwajumuisha tena wanajeshi watoto na mayatima wa vita katika jamii nchini Somalia.

Wakfu huo wa Ujerumani umejitolea kuimarisha ushirikiano kati ya Ujerumani na Afrika kwa miaka 45.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW