Makabiliano ya ICE, raia, yatikisa misingi ya Marekani
29 Januari 2026
Hatua zinazoonekana wazi kwa umma, wakati mwingine zenye kusababisha vifo na zinazoweza kukiuka Katiba, zinazotekelezwa na maafisa wa shirikisho la uhamiaji la Marekani, zinaweza kuwa zinabadilisha mtazamo wa Wamarekani kuhusu moja ya sera kuu za Rais Donald Trump.
Uhamiaji umekuwa nguzo muhimu ya ajenda ya kisiasa ya rais huyo kwa zaidi ya muongo mmoja wa maisha yake ya kisiasa, na ulikuwa kiini cha kampeni yake ya uchaguzi wa mwaka 2024.
Hata hivyo, tafiti za maoni ya umma zinaonyesha kuwa mitazamo ya wananchi imeanza kubadilika, kufuatia operesheni zilizosambazwa sana mitandaoni, zilizotekelezwa na maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) pamoja na mawakala wengine wa shirikisho katika maeneo ya mijini. Operesheni hizo mwezi huu zimesababisha vifo vya kupigwa risasi kwa raia wawili wa Marekani mjini Minneapolis.
Utafiti wa Reuters/Ipsos uliochapishwa Jumatatu kwa saa za huko, ukiwa umechukua maoni kabla na baada ya mauaji ya muuguzi wa wagonjwa mahututi (ICU) Alex Pretti, umeonyesha kuwa asilimia 53 ya Wamarekani hawaridhishwi na jinsi Trump anavyoshughulikia suala la uhamiaji. Hii ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na asilimia 39 waliokosoa sera hiyo siku ya kwanza ya muhula wake mpya mwezi Januari 2025. Waliompa ridhaa kuhusu sera zake za uhamiaji sasa ni asilimia 39, ikiwa ni kushuka kutoka kiwango cha juu cha asilimia 50 kilichorekodiwa Februari 2025.
Mgawanyiko wa kisiasa bado una mchango. Kwa ujumla, Warepublican waliunga mkono shughuli za ICE, huku zaidi ya Wademocrat tisa kati ya kumi wakipinga hatua hizo.
Hata hivyo, karibu theluthi mbili ya wapiga kura ambao hawakujitambulisha na chama chochote cha siasa walisema kuwa hatua za ICE zimevuka mipaka inayokubalika.
Kwa muda mrefu, ICE imekuwa na jukumu la kuwatambua na kuwakamata wahamiaji wasio na nyaraka halali. Lakini katika muhula wa pili wa Trump, shughuli za idara hiyo zimekabiliwa na maandamano, kampeni za uwajibikaji na ufuatiliaji wa umma, pamoja na kuongezeka kwa mvutano mitaani.
Hali hii ni mkusanyiko wa mambo kadhaa ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya uendeshaji wa ICE, kwa mujibu wa Kelsey Norman, mkurugenzi wa Mpango wa Haki za Wanawake, Haki za Binadamu na Wakimbizi katika Taasisi ya Baker ya Sera za Umma nchini Marekani.
Sababu hizo ni pamoja na kuwasili kwa maafisa wa ICE katika miji mikubwa, lengo binafsi la Trump la kufanikisha uhamisho wa watu milioni moja, ongezeko kubwa la bajeti ya idara hiyo na uajiri wa maafisa wapya, pamoja na kurekodiwa hadharani kwa vitendo vya vurugu — ambavyo sasa vimesababisha vifo — vikifanywa mitaani.
"Mbinu nyingi za kijeshi zimekuwepo ndani ya utekelezaji wa sheria za uhamiaji kwa muda mrefu,” Norman aliambia DW. "Kilichobadilika ni kwamba awali zilikuwa zikitumika zaidi mpakani, ambako hazikupata uangalizi wa umma kama zinavyopata sasa.”
Changamoto kwa maadili ya msingi ya Marekani
Vifo vya Renee Good na Alex Pretti vimeelekeza macho ya dunia katika operesheni za ICE ndani ya miji ya Marekani. (Pretti alipigwa risasi na kuuawa na maafisa wa Ulinzi wa Mpaka wakati wa maandamano dhidi ya ICE.) Kwa Wamarekani wa kawaida, operesheni hizi zinaangazia hatari nyingine kubwa — si tu uwezekano wa nguvu ya mauti kutumika dhidi ya raia.
Walter Olson, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Cato, taasisi ya utafiti ya mrengo wa uhuru wa soko nchini Marekani, alisema kuna ushahidi unaoonyesha kuwa hatua za ICE zinakiuka ulinzi wa kiraia unaolindwa na Katiba ya Marekani na Hati ya Haki (Bill of Rights).
Olson aliiambia DW kuwa kumekuwa na ukiukaji unaoonekana wa Marekebisho ya Nne ya Katiba, yanayohusu haki dhidi ya upekuzi na ukamataji usio halali, ambapo maafisa wa ICE wameingia katika nyumba za raia bila hati ya upekuzi iliyosainiwa na jaji. Aliongeza kuwa haki zinazolindwa kwa raia na wasio raia pia zimekiukwa.
"Tumeona ukiukaji kadhaa wa haki za upekuzi na ukamataji, ikiwemo kuvunja milango ya nyumba za watu,” Olson alisema. "Katika visa vingine, ambavyo ni vingi zaidi lakini havionekani kwa uzito ule ule, kanuni za kikatiba kuhusu lini polisi wanaweza kukusimamisha barabarani zimekiukwa.”
Kauli zilizotolewa baada ya kifo cha Pretti na maafisa wakuu wa utawala wa Trump pamoja na wafuasi wake pia zimeibua mjadala kuhusu Marekebisho ya Pili ya Katiba, yanayolinda haki ya kumiliki silaha.
Pretti alikuwa mmiliki halali wa silaha katika jimbo la Minnesota na alikuwa na ruhusa ya kubeba silaha iliyofichwa. Hata hivyo, hakuna hata moja ya video nyingi zilizorekodiwa na mashuhuda wa tukio hilo zinazoonyesha Pretti akitoa au kutumia silaha. Pamoja na hayo, baadhi ya viongozi wa utawala walisema kuwa hakupaswa kubeba silaha wakati wa maandamano. Hoja hii imepingwa hata ndani ya Chama cha Republican na miongoni mwa wahafidhina, wakisisitiza ulinzi wa kikatiba.
"Marekebisho ya Pili ya Katiba yamekuwa yakithaminiwa sana na wahafidhina wa Marekani kwa miongo mingi,” Olson alisema.
"Lakini utawala wa Trump ulitoka na kusema mambo kama vile hupaswi kubeba silaha mitaani au katika maandamano — hata kama, kama ilivyokuwa Minnesota, sheria ya jimbo inaruhusu, hata kama una leseni ya kubeba silaha iliyofichwa, na hata kama hujawahi kuitoa au kuitishia mtu.”
"Hii ni mabadiliko makubwa kabisa, ya nyuzi 180, kutoka msimamo wa awali wa kihafidhina,” aliongeza.
Alisema pia kuwa raia wa Marekani huenda sasa wanaanza kujiuliza hatua hizi zinaashiria nini kwa siku zijazo.
"Kwa Wamarekani wa kawaida, swali wanapaswa kujiuliza ni hili: ikiwa haya yanaweza kufanywa katika kampeni dhidi ya wahamiaji, ni wapi pengine yanaweza kufanywa pale kampeni itakapogeukia watu wanaochukuliwa kuwa wasaliti au ‘wasio Wamarekani'?” Olson alisema.
Hatua zisizo za kawaida katika demokrasia
Ingawa jukumu na mamlaka ya ICE yamebadilika katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 ya kuwepo kwake, mwenendo wa idara hiyo katika muhula wa sasa wa Trump hauna mfano wake — si tu Marekani bali pia katika demokrasia nyingine, Norman alisema.
Awali, chini ya tawala zilizopita ikiwemo muhula wa kwanza wa Trump, ICE ilifanya shughuli zake zaidi mpakani na kwa kiasi kikubwa nje ya macho ya umma. Sasa, kuhamia katika miji ya kaskazini kumeleta maafisa wa shirikisho waliovaa nyuso zilizofunikwa katikati ya maeneo yenye watu wengi, ambako karibu kila mtu ana simu ya kurekodi.
Hilo limewezesha shughuli zao kufuatiliwa, kurekodiwa, na kuchunguzwa kwa karibu zaidi, na kufichua mbinu kali zinazotumiwa na baadhi ya maafisa wake.
"Mbinu ambazo ICE inatumia ni zile ungetarajia kuona zikitekelezwa na polisi katika nchi zenye mifumo ya kiimla,” Norman alisema.
Matumizi ya nguvu, yakiwemo gesi ya kutoa machozi na pilipili, dhidi ya mashuhuda na makundi ya kiraia yanayodai uwajibikaji, pia yamevuta hisia za mashirika ya kimataifa ya usimamizi wa polisi, ikiwemo Chama cha Kimataifa cha Wakuu wa Polisi.
Shirika hilo lilitoa tamko likiitaka Ikulu ya White House kuwaleta pamoja viongozi wa utekelezaji wa sheria katika ngazi zote ili "kusaidia ushirikiano wa utulivu, unaozingatia sheria, na sera zinazotegemea mbinu zilizothibitika.”
Wachunguzi pia wamewahi kuonya kuwa kampeni kubwa ya kuajiri maafisa wapya inaweza kuwa inasababisha baadhi ya maafisa wa ICE kufanya kazi bila mafunzo ya kutosha.
Mvutano wa sasa unaweza kubadilisha mtazamo wa umma kuhusu ubora na weledi wa karibu mashirika 18,000 ya utekelezaji wa sheria nchini Marekani, alisema Kathy O'Toole, mshirika katika kampuni ya ushauri ya 21CP Solutions, iliyoanzishwa kufuatia tathmini ya sera za polisi wakati wa utawala wa Obama.
O'Toole, ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa polisi mjini Boston na Seattle, alisema polisi wa maeneo ya ndani huenda wakalazimika kubeba mzigo wa athari za utata unaoihusisha ICE.
"Katika miji mikubwa kadhaa sasa, kuna mvutano mkubwa kati ya polisi wa shirikisho na wa ndani kiasi kwamba hali hiyo hainufaishi mtu yeyote,” O'Toole aliiambia DW.
"Ikitokea janga katika jamii mikononi mwa vyombo vya dola, wananchi hawatofautishi kati ya polisi wa shirikisho na wa jimbo au wa eneo. Kinachoonekana sasa Minneapolis na miji mingine mikubwa, ni kwamba polisi wa ndani ndio wanaobaki kukabiliana na athari za maandamano hayo,” alisema.