1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu zaiendelea Ufaransa kulaani kifo cha kijana Nahel

30 Juni 2023

Maandamano makubwa yameitikisa Ufaransa usiku wa kuamkia leo ikiwa ni siku ya tatu mfululizo kufuatia kifo cha kijana mmoja aliyepigwa risasi na polisi mapema wiki hii.

Polisi karibu na gari lililochomwa moto
Maelfu ya polisi wametawanywa nchi nzima kuzima vurugu zinazoendelea UfaransaPicha: Gonzalo Fuentes/REUTERS

Ufaransa imeshuhudia usiku mwingine wa vurugu za kutisha ambapo maelfu ya watu wameteremka mitaani kulaani kifo cha kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17 aliyepigwa risasi na polisi siku ya Jumanne.

Kifo cha kijana huyo aliyetambulishwa kwa jina moja la Nahel, kimetonesha kidonda cha hasira miongoni mwa Wafaransa juu ya jinsi polisi ya nchi hiyo inavyofanya kazi na madai ya ubaguzi unaozilenga jamii za wasio wazungu.

Waandamanaji hawakujali idadi kubwa ya polisi waliotawanywa mitaani na badala yake wamefanya vurugu na uharibifu wa kila aina kulaani kisa hicho cha mauaji.

Maduka yameporwa, magari yamechomwa moto na polisi wameshambuliwa kwa mabomu ya kienyeji yanayotengenezwa kwa chupa, utambi na mafuta ya petroli.

Ghasia za kulaani kifo cha Nahel ziripotiwa ndani na nje ya Ufaransa 

Vurugu kubwa zimeripotiwa mjini Paris hususani kwenye kitongoji cha Nanterreeneo ambako polisi mmoja alimpiga risasi Nahel baada ya kumsimamisha barabarani kwa ukaguzi wa kawaida.

Mji Mkuu Paris ndiyo kitovu cha ghasia za kulaani kifo cha Nahel Picha: Aurelien Morissard/AP/picture alliance

Tawi moja la benki limechomwa moto na jengo la juu pia lilishika moto ambao hata hivyo ulizimwa bila ya kuwa na madhara makubwa.

Katika mwa mji huo mkuu maduka kadhaa ya bidhaa za fahari yalilengwa na waandamanaji walipofanya uporaji. 

Kwa ujumla usiku wa kuamkia leo mji wa Paris na viunga vyake uligeuka uwanja wa mapambano kati ya polisi na waandamanaji inaosemekana walichanganyika na magenge ya wahalifu.

Hali ya vurumai imeshuhudiwa vilevile kwenye miji mingine ya Ufaransa tangu Marseille, Lyon, Pau, Toulouse na Lille.

Maandamano ya kulaani mauaji ya Nahel yamefanyika pia nchi jirani ya Ubelgiji ambako watu 30 wamekamatwa kwa kufanya vurugu. 

Mama wa Nahel asema lawama zake zinakwenda kwa polisi aliyefyetua risasi 

Mkusanyiko wa kudai haki kwa Nahel, kijana aliyeuwawa na polisi wa Ufaransa Picha: Michel Euler/AP Photo/picture alliance

Akizungumza kwa mara ya kwanza katika mahojiano ya televisheni, mama wa Nahel anayeitwa Mounia amesema hailaumu polisi nzima kwa kifo cha mtoto wake bali anaelekeza machungu yake kwa afisa mmoja pekee aliyefanya kitendo hicho.

Mama wa Nahel amesema polisi huyo alimuona mtoto wake kwa jicho la kuwa ni mwarabu, tena mwenye umri mdogo na hivyo akaamua kuchukua maisha yake.

Afisa anayedhaniwa kufanya mauaji hayo huenda atafunguliwa mashtaka ya kuua kwa kukusudia. Waendesha mashtaka wanasema hakuzingatia kanuni za matumizi ya silaha ya moto.

Inaarifiwa siku ya tukio, kijana aliyeuwawa alisimamishwa na polisi kwa makosa ya kuendesha gari kwa mwendo mkubwa. Walimtaka kuzima chombo hicho, lakini  ghafla kijana huyo aliondoa gari lake haraka na hapo ndipo afisa anayechunguzwa alifyetua risasi iliyomuua.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameutaja mkasa huo kuwa "usiosameheka" lakini amewataka waandamanaji kusitisha vurugu akisema matendo yao "hayakubaliki".

Vurugu hizo ni changamoto mpya kwa utawala wa Macron ambaye anajaribu kuirejesha nchi kwenye utulivu baada ya wimbi jingine kubwa la maandamano yaliyochochewa hivi karibuni na maguezi ya mfumo wa pensheni. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW