1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

VURUGU ZATAWALA KAMPENI PAKISTAN

Liongo, Aboubakary Jumaa13 Februari 2008

Kuendelea kwa ghasia na mapigano nchini Paksitan , kabla ya uchaguzi mkuu, Jumatatu ijayo, kumevifanya vyama vya siasa kushindwa kufanya kampeni vizuri.

Mkaazi wa Pakistani akipita mbele ya bango la kampeni la kiongozi wa upinzani Nawaz Sharif mjini Lahore.Picha: AP

Kwa upande mwengine viongozi wa vyama vikuu vya upinzani wakubaliana kushirikiana mara baada ya uchaguzi huo bila ya kujali chama gani kuitashinda.


Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanasema kuwa pamoja na kuwa imebaki wiki moja kabla ya uchaguzi huo lakini ile homa ya uchaguzi haipo.


Hashim Khan ambaye ni mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika chuo kikuu cha Peshawar anasema kuwa kabla ya kuawa kwa Bi Benazir Bhutto tarehe 27 Decemba mwaka jana, homa ya uchaguzi ilikuwa imepanda tofauti na ilivyo hivi sasa.


Mikutano ya kampeni imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga.


Mfano katika mkutano wa kampeni wa chama  Awami National cha ANP huko kusini katika jimbo lenye ghasia nyingi la Waziristan tarehe 11 mwezi huu, watu sita waliauawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, miongoni mwao akiwa mgombea wa chama hicho, Mohammad Nisar Khan.Hiyo ilikuwa ni baada ya shambulizi la bomu.


Rais wa chama hicho cha ANP Asfandyar Wali Khan ambaye ilikuwa ahutubie katika mkutano huo, alisema kuwa shambulizi hilo lilikuwa jaribio la kutaka kuusambaratisha kabisa uongozi wa chama chake ili uchaguzi uahirishwe tena.


Siku mbili kabla ya hapo watu 25 waliuawa na zaidi ya 40 kujeruhiwa baada ya bomu kutupwa kwenye mkutano wa kampeni wa chama cha NWFP uliyofanyika kwenye wilaya ya Charsadda.


Tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi nyingine sita zilizopita, ambapo mikutano ya kampeni ilikuwa ikifanyika katika maeneo wazi na kuvutia watu wengi, safari hii wagombea wamekwepa aina hiyo ya kampeni.


Hivi sasa wamekuwa na mikutano ya ndani na kuendesha kampeni zao nyumba kwa nyumba wakihofu kushambuliwa na watu wakujitoa mhanga.


Maeneo ya mipakani nchini humo yamekuwa yakikabiliwa na ghasia na mauaji toka majeshi ya Marekani yalipoanzisha harakati maalum dhidi ya ugaidi nchini Afghanistan, kufuatia shambulizi la septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.


Wanamgambo wa Kitaliban na wale wa al Qaida wamekuwa na hifadhi katika maeneo yanayotawaliwa kikabila kama vile jimbo la Waziristan ambako inaaminika w ashambuliaji wengi wa kujitoa mhanga wamekuwa wakipata mafunzo yao.


Arshad Ali ambaye ni mtafiti katika chuo kikuu cha Peshawar anaamini kuwa wanamgambo wa kitalibaN wanachangakia kwa kiasi kikubwa katika mashambulizi hayo.


Katika hatua nyingine vyama viwili vikubwa vya upinzani nchini humo vimekubaliana kushirikiana mara baada ya uchaguzi huo.


Asif Ali Zardari ambaye ni mume wa aliyekuwa kiongozi cha kikuu cha upizani  cha PPP,Bi Benazir Bhutto amekubaliana na kiongozi wa chama cha Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Shariff kushirikiana bila ya kujali ni chama gani kitashinda.


Kura za maoni zinaonesha kuwa upinzani huko mbele ya chama kinachoungwa mkono na Rais Pervez Musharraf PML.


Kura hizo zimeonesha kuwa chama cha Hayati Bhutto cha PPP ni maarufu zaidi zaidi kuliko vingine toka alipouawa kiongozi wake huyo.


Hapo jana Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa  ukielezea wasi wasi wake juu ya uchaguzi huo na kuzitaka mamlaka za nchi hiyo kuimarisha mazingira ya kuufanya uwe huru na haki.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW