1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuta nikuvute baada ya ushindi wa Hamas

Oummilkheir31 Januari 2006

Hamas wanaitaka jumuia ya kimataifa iendelee kuwasaidia wapalastina lakini bila ya masharti

Kiongozi mkakamavu wa Hamas Khaled Machaal
Kiongozi mkakamavu wa Hamas Khaled MachaalPicha: AP

Muda mfupi baada ya pande nne zinazosimamia utaratibu wa amani kutoa taarifa inayoshurutusha misaada kwa Palastina na kutambuliwa na Hamas taifa la Israel pamoja pia na kusitisha matumizi ya nguvu,Rashia imejitokeza na hoja zinazopingana na hizo.Na Hamas pia wameyakataa masharti yaliyotolewa.

Hamas imesema hii leo msaada wa kimataifa haustahiki kufungamanishwa na masharti.Mkuu wa Hamas Ismael Haniyeh amesema tunanukuu:”Msaada wa kimataifa kwa umma wa Palastina ni wajib kwasababu wapalastina wanajikuta bado wanaishi chini ya uvamizi wa Israel.”Mwisho wa kumnukuu kiongozi huyo wa Hamas.

Wakikutana mjini London jana,wanadiplomasia wa pande nne zinazosimamia utaratibu wa amani ya mashariki ya kati,yaani Marekani,Rashia,Umoja wa mataifa na Umoja wa ulaya walishurutisha misaada ya siku za mbele kwa utawala wa ndani wa Palastina na kutambuliwa Israel na Hamas , kuachana na matumizi ya nguvu na kuheshimu makubaliano yote yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na mpango mpya wa amani ya mashariki ya kati.

Muakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa ulaya Javier Solana amesisitiza masharti hayo yakikubaliwa ndipo jumuia ya kimataifa itakapoendelea kuwasaidia wapalastina.

Licha ya kuyakosoa masharti hayo,mkuu wa Hamas Ismael Haniyeh amekwepa kujibwaga katika mvutano pamoja na jumuia ya kimataifa japo kama anaendelea kushikilia msimamo wa chama chake.Amesema ”Hamas imeingia madarakani kupitia uchaguzi huru na wa haki na sio kwa mtutu wa bunduki au kwa mapinduzi ya kijeshi.”

Ismael Haniyeh anahoji dhamiri ya kusitisha misaada ya kimataifa haitawazuwia wafadhili wengine muhimu kuonyesha hamu ya kutaka kuwasaidia wapalastina.Hakuwataja lakini wafadhili wenyewe.

Matamshi makali zaidi yametolewa na kiongozi wa Hamas anaeishi uhamishoni Khaled Mechaal aliyesema kupitia gazeti la Guardian kwamba chama chake hakitaacha mapambano na “hakitakubali kutiwa kishindo na Marekani na umoja wa Ulaya”.

Taarifa ya pande nne iliyotangazwa mjini London haijakawia kunyunyiziwa mchanga na Rashia.Rais Vladimir Putin amesema hii leo jumuia ya kimataifa inapaswa kuendelea kuwasaidia wapalastina,licha ya ushindi wa Hamas.

Rais Putin amesema tunanukuu:

“Tunahisi,kwa kila hali , kutowapatia wapalastina msaada ni makosa.”Mwisho wa kumnukuu rais Putin aliyesema pia msimamo wa chama chake kuelekea Hamas haulingani na ule wa Marekani au wa Umoja wa ulaya.

Wakati huo huo chama cha Kadima kinapanga kutangaza orodha ya watetezi wa uchaguzi mkuu baadae hii leo.Orodha hiyo inaongozwa na waziri mkuu wa ampito Ehud Olmert akifuatiwa na waziri mkuu wa zamani wa chama cha Labour Shimon Perez na waziri wa mambo ya nchi za nje bibi Tzipi Livni.

Kampeni ya uchaguzi wa March 28 ijayo inaanza rasmi hii leo nchini Israel.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW