1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuta nikuvute kuhusu bima ya Afya 'Obamacare'

4 Januari 2017

Obama apanga kukutana na wabunge katika juhudi za kuwarai kuunga mkono bima hiyo ya afya. Rais Mteule Donald Trump na baadhi ya wabunge wa Republicans wameapa kufanya haraka iwezekanavyo kuifutilia mbali bima hiyo.

USA | US-Präsident ObamaPressekonferenz Jahresrückblick
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Rais wa Marekani, Barrack Obama anatarajiwa kufanya ziara fupi ya kisiasa kuelekea katika jengo la bunge la Marekani, Capitol Hill kuwarai wabunge kuunga mkono bima ya afya aliyoanzisha iitwayo Obama Care ambayo alisaini kwa mujibu wa sheria. Atakutana na maseneta na wabunge wa chama cha Democratic kujadili namna ya kulikabili lengo la Warepublicans kutaka bima hiyo iondolewe. 

Kampeni ya miaka minane ya utawala wa Rais Barrack Obama kutaka kuendeleza utoaji wa bima ya afya kwa makumi ya mamilioni ya Wamarekani, itakumbwa na pigo baada ya pigo punde rais Mteule Donald Trump achukuapo usukani tarehe 20 mwezi huu, hasa ikizingatiwa Warepublican ndio wengi zaidi katika mabunge mawili nchini humo.

Juhudi za Obama zinajiri wakati Rais Mteule Donald Trump na baadhi ya wabunge wa Republicans wameapa kufanya haraka iwezekanavyo kuifutilia mbali bima hiyo. Makamu wa rais mteule Mike Pence amesema atakutana leo na wabunge kujadili mustakabali wa nchi. Hili hapa tamko la Pence kuhusu bima ya Afya ya Obama ''Tutakutana na wajumbe wa bunge na seneti kujadiliana namna ya kusogeza mbele ajenda ya kuiimarisha tena Marekani. Tutalenga kuondoa bima ya Obama Care na kuibadilisha na nyingine. Tunatumai kutunga kipengee cha sheria kitakachotuwezesha kuondoa vizingiti ambavyo vimekuwa vikilemaza ukuaji wa ajira na maendeleo.''

Rais Mteule Donald Trump (kushoto) na Makamu wa Rais Mteule Mike Pence (kulia)Picha: Reuters/M. Segar

Baada ya uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka jana, Wademocrats wamezidiwa idadi bungeni, na hivyo huenda wanazo nafasi chache sana kufaulu kupinga mageuzi bila ya wanachama wa Republican kuwaunga mkono.

Kadhalika wanakosolewa kwamba mageuzi ya Obama yamechangia kuongezeka kwa ada za bima kando na matatizo mengine.

Hata hivyo, japo suala la Warepublican kupinga bima hiyo ni dhahiri, bado hawana suluhisho mbadala. Spika wa Bunge Paul Ryan amependekeza mfumo wa kodi kwa mikopo, lakini gharama kwa serikali na raia bado hazieleweki.

Wengine wamependekeza kuwa bima hiyo iondolewe sasa, lakini irejeshwe labda baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Maafisa katika Ikulu ya White House wanaamini kuwa Wamarekani watatoa hisia za ghadhabu endapo Trump ataifuta bima hiyo inayowasaidia mamilioni ya watu wasiojiweza kupata huduma za afya, bila ya kuwapa suluhisho mbadala.

Wanatumai kuwa kilio cha umma huenda kikamlazimisha Trump kuchukua mkondo wa kuifanyia mageuzi muhimu ambayo baadhi yamependekezwa na wanachama wake.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW