1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

VW yaamuriwa kulipa fidia kashfa ya 'dieselgate'

25 Mei 2020

Mahakama ya juu ya kiraia nchini Ujerumani imehukumu dhidi ya Volkswagen, katika kesi ya kwanza iliyofunguliwa na mmiliki wa gari dhidi ya kampuni hiyo ya magari kuhusu udanganyifu wa vipimo vya uchafuzi wa mazingira.

Deutschland Symbolbild VW-Abgasskandal
Picha: picture alliance/dpa/J. Stratenschulte

Mahakama kuu ya kiraia nchini Ujerumani imepitisha uamuzi dhidi ya kampuni ya Magari ya Volkswagen katika kesi ya kwanza iliyowasilishwa na mtumiaji gari ya kampuni hiyo kufuatia suala zima la udanganyifu wa vipimo vya kiwango cha moshi unaotoka kwenye magari. Uamuzi huu umefungua njia kwa maelfu ya kesi nyingine zaidi kuelekea kampuni hiyo.

Mahakama ya haki ya shirikisho siku ya Jumatatu 25.05.2020 imepitisha uamuzi dhidi ya kampuni hiyo ya Kijerumani ya Volkswagen katika kesi ya kwanza nchini humo iliyofunguliwa na mmiliki mmoja wa gari ya kampuni hiyo.

Mahakama imesema kwamba watu walionunua magari ya Volkwagen yaliyowekwa programu maalum ambayo inachezea vipimo vya kiwango cha moshi wa gari wanastahili kulipwa fidia ya kifedha.

Mwakilishi wa upande wa utetezi Herbert Gilbert akiwa katika chumba cha mahakama wakati majaji wakiwasili kwa ajili ya kutoa hukumu yao katika kesi dhidi ya Volkswagenm Mei 25, 2020.Picha: Reuters/T. Gutschalk

Watu hao wanaweza kuyarudisha magari na kurudishiwa kiwango fulani cha fedha kutoka kampuni hiyo. Aidha katika utaratibu uliopo kiwango cha kilomita zilizotumika kitazingatiwa wakati wa wateja hao kuhesabiwa fidia yao kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama hiyo.

Jaji Stephan Seiters aliyetowa uamuzi wa Jumatatu, alisema tabia ya washtakiwa yaani kampuni ya Volkswagen haikuendana na maadili. Kampuni hiyo ya magari ya kijerumani imeahidi kutoa kiwango kinachostahili kwa wale walioathirika ikisema sasa inalenga kuzifikisha mwisho hivi karibuni kesi hizi katika makubaliano na wadai.

Kashfa ya Volwagen hasa ikoje?

Mwezi Septemba mwaka 2015,Volkswagen ilikiri mbele ya shirika la Marekani la kulinda mazingira kwamba iliweka kifaa malum katika magari milioni 11 dunia nzima ambacho kitawezesha udanganyifu kufanyika katika upimaji viwango vya gesi inayotoka kwenye magari hayo.

Wanasayansi wa Marekani walikigundua kifaa hicho kilichowekwa kwenye magari ya VW ambacho kilikuwa na uwezo wa kugundua vipimo vya moshi katika mazingira mbali mbali na kiliweza kubadili uwezo wa gari kwa mujibu wa mazingira yaliyopo ili kuimarisha matokeo ya kipimo hicho.

Injini ya gari aina ya Volkswagen Touran ambayo ni mojawapo ya yaliohusika katika kashfa ya udanganyifu wa vipimo vya uchafuzi wa mazingira.Picha: Julian Stratenschulte/dpa/picture alliance

Kashfa hii ilipewa jila la ''Dieselgate'' na ilisababisha mgogoro mkubwa katika imani ya wateja kuelekea sekta nzima ya magari baada ya visa vingine vya kashfa inayofanana na hiyo kugundulika baadae kwenye makampuni mengine. Tangu wakati huo VW imejikuta imefungwa mikono katika mchakato wa kisheria.

Maamuzi ya kimahakama

Mahakama pia imeamrisha makampuni mengine ya magari yaliyohusika katika kashfa hii kulipa faini na kuyarudisha maelfu ya magari yanayoaminika yaliweka softaware au kifaa hicho cha udanganyifu.

Waendesha mashtaka wa Ujerumani pia waliwasilisha mashtaka dhidi ya watendaji wakuu wa VolksWagen kuhusiana na kadhia hiyo. Mkurugenzi mkuu mtendaji Herbert Diess na mkuu wa bodi ya usimamizi Hans Diter Poetsch walikubali mwezi Mei kulimaliza suala hili nje ya mahakama kwa kulipa yuro milioni tisa.

Kinachofuata.

Kiasi kesi 60,000 za watu binfsi dhidi ya kampuni hiyo ya magari ya Ujerumani zipo mahakamani hivi sasa kwa mujibu wa Volkwagen.Mahakama za chini za Ujerumani zinafuata maamuzi yanayochukuliwa na mahakama ya juu,na kwa manaa hiyo uamuzi uliotolewa unaongeza kwa kiasi kikubwa nafasi ya wamiliki wa magari kushinda kesi zao,hatua ambayo huenda ikawafanya kulipwa na kampuni iliyotengeneza magari hayo.

Chanzo: DW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW