1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama rafiki na Urusi Ujerumani vyapata mafanikio

Sylvia Mwehozi
2 Septemba 2024

Chama cha siasa kali za mrengo mkali wa kulia Ujerumani cha AfD na chama cha kizalendo cha muungano wa Sahra Wagenknecht BSW vyote vimepata mafanikio katika uchaguzi wa majimbo wa Septemba Mosi.

Siasa | Bendera ya Ujerumani na ya AfD
Bendera ya Ujerumani na ya chama cha AfD naPicha: Andreas Arnold/dpa/picture alliance

Sahra Wagenknecht na chama chake kipya alichokianzisha cha BSW ni mkosoaji mkubwa wa ushiriki wa kijeshi na ilani yake inasema vita vinachochea hofu na kusababisha ukosefu wa utulivu.

Kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, chama hicho kinaishutumu Marekani na Jumuiya ya Kujihami NATO na kinataka kuijumuisha Urusi katika mfumo wa usalama wa Ulaya.

BSW ni chama cha kizalendo ambacho kinajumuisha sera za kiuchumi zinazoegemea mrengo wa kushoto, uhamiaji wa kihafidhina na mipango ya sera ya kigeni inayounga mkono Urusi.

Moja ya mada kuu za chama hicho ni ukosoaji mkali wa msaada wa kijeshi unaotolewa na Ulaya na Marekani kwa Ukraine. Katika uchaguzi wa majimbo mawili ya mashariki ya Thuringia na Saxony, BSW ilishinda kwa karibu asilimia 16 na 12.

Ukaribu wa jadi na Urusi

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Ujerumani AfD pia kimeangazia sana vita vya Ukraine katika kampeni zake za uchaguzi katika majimbo ya mashariki. AfD inataka kusitishwa kwa msaada wa kijeshi wa Ujerumani kwa Ukraine.

Wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alipotoa wito kwa bunge la Ujerumani Bundestag mnamo Juni mwaka huu wa kupatiwa msaada zaidi kwa nchi yake, idadi kubwa ya wabunge wa AfD waliondoka ndani ya bunge kama ilivyokuwa kwa wanachama wa BSW.

Mwenyekiti wa AfD wa wilaya ya Chemnitz huko Saxony, Nico Köhler, aliiambia DW kuwa anadhani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ulikuwa sahihi, lakini NATO na Marekani zinahusika kwa kiasi fulani.

Uungwaji mkono wa AfD mashariki mwa Ujerumani

03:05

This browser does not support the video element.

Soma pia:Serikali ya muungano ya Ujerumani kuyumbishwa na matokeo ya majimbo

Mwanasiasa wa AfD Björn Höcke anaenda mbali haswa katika shauku yake ya kujongeleana na rais wa Urusi Vladimir Putin. Höcke anachukuliwa kuwa mmoja wa wanasiasa wa Ujerumani wenye msimamo mkali.

Katika toleo la Januari 2023 la mijadala ya Maximilian Krah wa AfD "Dresdner Gespräche"  ama mazungumzo ya Dresden, Höcke alitoa maoni kuhusu Urusi chini ya Putin:

Alisema kwamba "Urusi, iwe vyombo vya habari vitataka kusikia au la ni nchi ambayo sio tu inachochea vyama lakini pia ni nchi ambayo inatumai kuwa inaweza kuwa mwanzilishi wa ulimwengu wa mataifa huru na bila ushawishi wenye nguvu."

Je, ni kweli kwamba Urusi ni kinara wa mataifa yaliyo huru?

Mwanahistoria Ilko-Sascha Kowalczuk anaonya hata hivyo juu ya kuimarika kwa vyama kama vile AfD na BSW. Aliileza DW kuwa "siyo kwamba kwa namna fulani wanamwona Putin kama mwokozi pia wanajua kwamba yeye ni dikteta mwenye kiu ya kumwaga damu".

Kowalczuk ana hakika kwamba AfD na BSW zimeathiriwa na sera za chama cha kiimla cha Socialist Unity Party of Germany SED, kilichotawala Ujerumani Mashariki hadi nchi hiyo ilipoungana tena.

Kama Putin, AfD na BSW zinakataa mabadiliko mengi ya kijamii ya miaka ya hivi karibuni. Wote wana shaka na masuala kama vile uhamiaji na Uislamu na mijadala kuhusu jinsia na vuguvugu la LGBTQ+.

Soma pia:Ujerumani: AfD ya mrengo wa kulia yatafuta mafanikio katika kura ya Saxony, Thuringia

Miaka 25 ya Putin madarakani na ushawishi wa Urusi Afrika

02:17

This browser does not support the video element.

Vyama vyote viwili vinaonekana kunufaika ukosefu wa imani katika serikali ya muungano wa vyama vitatu ya Kansela Olaf Scholz.

Hata kama uchaguzi wa majimbo hautakuwa na athari za moja kwa moja kwa sera ya kigeni ya Ujerumani au sera ya uhamiaji, kuimarika kwa AfD na BSW kunaweza kuongeza shinikizo kwa watunga sera kufikiria upya uungaji mkono wake kwa Ukraine.