1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama Ujerumani kuanza mazungumzo kuunda serikali ya mseto

27 Septemba 2021

Vyama vinne vya Ujerumani vinajiandaa kwa mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano baada ya matokeo ya uchaguzi wa Jumapili kuonesha chama cha SPD kimepata ushindi mwembamba dhidi ya muungano wa kihafidhina wa CDU/CSU.

Deutschland Bundestagswahl 2021, SPD feiert die Sieger
Picha: Nina Haase/DW

Chama cha siasa za mrengo wa kati kushoto SPD kilipata asilimia 25.7, hayo yakiwa matokeo yake bora zaidi katika miaka mingi. Kwa pande mwingine muungano wa kihafidhina CDU/CSU wa kansela anayeondoka Angela Merkel na ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 16, ulipata matokeo mabaya ya asilimia 24.1.

Wagombea wawili wakuu wa vyama hivyo vilivyoshika nafasi ya kwanza na pili Olaf Scholz wa SPD na Armin Laschet wa CDU wamesema wanataka kuunda serikali ijayo.

Soma pia: Ujerumani kuwa na serikali nyengine ya mseto

Scholz anayo nafasi nzuri zaidi ya kufanya hivyo, lakini katiba ya Ujerumani pia inatoa nafasi kwa chama cha pili  kwa ukubwa pia kuunda serikali.

Huyu hapa Scholz mwenye umri wa miaka 63 akizungumza na wanachama wake katika makao makuu ya chama hicho kuhusu matarajio yao kuunda serikali.

“Wapiga kura wamejieleza bayana. Wamesema nani anapaswa kuunda serikali ijayo. Wameimarisha vyama vitatu: Chama cha kidemokrasia cha mrengo wa kati kushoto, chama cha Kijani na FDP. Ka hivyo huo ni wajibu wa wazi ambao umetolewa na raia wa nchi hii. Vyama hivyo vitatu vinapaswa kuunda serikali," amesema Scholz.

Mgombea ukansela wa CDU(CSU Armin Laschet.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Armin ajikuta kwenye shinikizo ndani ya chama chake

Katika kambi ya wahafidhina, mgombea ukansela wa CDU/CSU Armin Laschet amekuwa akijaribu kujinusuru kisiasa. Wachambuzi wanasema uungwaji wake mkono unapungua kwa kasi miongoni mwa wakuu wa muungano huo, kufuatia kampeni ilokumbwa na mushkil na kusababisha muungano huo kupata matokeo mabaya zaidi katika historia yake.

Soma pia: Maoni: Kubalini, Ujerumani inataka mabadiliko

Vyama vingine viwili vitakuwa na nafasi mkubwa katika kuamua serikali ijayo ya mseto. Navyo ni chama cha Kijani cha watetezi wa mazingira ambacho kilijizolea asilimia 14.8 ya kura na chama kinachowapendelea wafanyabiashara FDP ambacho kilipata asilimia 11.5.

Olaf Scholz ambaye ni waziri wa sasa wa Fedha na amesema pia kwamba muungano wa CDU/CSU unapaswa kupelekwa kwenye upinzani kwa kuwa umeshindwa na umepokea ujumbe kutoka kwa raia kwamba hawapaswi kuwa serikalini tena

Hayo yakijiri, mkuu wa bunge la Umoja wa Ulaya David Sassoli amempongeza Olaf Scholz kwa ushindi wake. Sassoli ndiye afisa wa kwanza wa Umoja wa Ulaya kutoa pongezi kwa Scholz.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Sassoli amesema baada ya hali hii tete ambayo ni ya kihistoria, hakuna muda wa kupoteza. Ulaya inahitaji mshirika imara mjini Berlin ili kuendelea na kazi.

Chama cha Kijani cha watetezi wa mazingira ni miongoni mwa vyama vilivyo na nafasi kubwa kuamua nani ataunda serikali mpya.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Mazungumzo ya vyama kuunda serikali mpya kuanza Berlin

Ili kuepusha serikali nyingine ya mseto kama iliyoko madarakani kwa sasa chini ya uongozi wa Merkel, muungano wa CDU/CSU pamoja na chama cha SPD vitalazimika kuvishawishi vyama vya Kijani na FDP kuungana navyo ili kuwa na serikali ya mseto yenye vyama vitatu. Tatizo ni kwamba baadhi ya ajenda za vyama hivyo vinatofautiana kisiasa.

Wawakilishi wa chama cha Kijani pamoja na wale wa FDP walitarajiwa kukutana ili kuafikiana kuelekea kwenye mazungumzo na vyama viwili vikuu kuhusu uundaji wa serikali

Baraza jipya lijalo la mawaziri litakuwa la kwanza katika miaka 16 iliyopita kutoongozwa na Angela Merkel. Mabadiliko hayo ambayo huenda yatachukua wiki au hata miezi kadhaa yatakuwa ya kihistoria.

(DPAE, RTRE, AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW