1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahafidhina washikilia viti vingi bunge la Ulaya

10 Juni 2024

Ushindi wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa na Ujerumani, haujaweza kuvipindua vyama vya kihafidhina vyenye wingi wa viti katika bunge la Ulaya.

Uchaguzi wa bunge la Ulaya
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akifurahia ushindi wa vyama vinavyounga mkono Umoja wa UlayaPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP/dpa/picture alliance

Ingawa vyama vikuu vya kihafidhina vimepata ushindi wa jumla katika bunge la Ulaya, lakini katika maeneo mengi ya Umoja huo vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vimepata mafanikio makubwa katika uchaguzi huo uliomalizika Jumapili. Vyama hivyo vimeibuka katika nafasi ya kwanza nchini Ufaransa, Italia na Austria na nchini Ujerumani na Uholanzi vimeshika nafasi ya pili.

Nchini Ujerumani, chama cha Kansela Olaf Scholz cha SPD kimepata pigo baada ya kuibuka nafasi ya tatu, hayo yakiwa ni matokeo mabaya sana katika uchaguzi wa Ulaya. Mojawapo ya chama mshirika katika muungano wake chama cha kijani, pia kilipata pigo kubwa kwa kupoteza viti 10 kati ya 25 kwenye bunge la Ulaya. Kote Ulaya, vyama vya kijani havikuweza kuendeleza rekodi yake ya kunyakua viti vingi kama ilivyokuwa uchaguzi wa 2019.

Mwanasiasa wa chama cha National Rally cha Ufaransa Marine Le Pen Picha: Andre Pain/EPA

Vyama vya siasa kali vyaungwa mkono

Nchini Italia, Chama tawala cha udugu wa Italia cha waziri mkuu Giorgia Meloni kimefanya vizuri zaidi kuliko ilivyotabiriwa, kikitoka na asilimia 28. Matokeo hayo yanamfanya Meloni kuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa Ulaya kuibuka kidedea katika uchaguzi huo. Nchini Austria, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Freedom kinaongoza kulingana na kura zilizohesabiwa, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kundi hilo kuongoza katika kura za nchi nzima.

Soma: Wapiga kura wahitimisha uchaguzi wa bunge la Ulaya

Huko Hungary, matokeo ya mwisho yanaonyesha chama cha waziri mkuu Viktor Orban cha mrengo wa kulia cha Fidesz kinaelekea kupoteza viti katika utawala wake wa miaka 14, japo bado kina asilimia 44 lakini ni chini ya asilimia 52 kilichoshinda mnamo 2019.

Kulingana na matokeo ya awali ambayo yametolewa, kundi la vyama vinayopigia upatu Umoja wa Ulaya limeshinda viti 191 kati ya viti 720 katika nchi zote wanachama 27 za muungano huo.

Fahamu kuhusu uchaguzi wa Bunge la Ulaya

01:24

This browser does not support the video element.

Katika nafasi ya pili kunafatiwa na kundi la vyama vilivyodhoofika vya mrengo wa kushoto vyama vya Kisosholisti vikiwa na wabunge 135 na kufuatiwa na kundi la kiliberali lenye wabunge 83. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, hapa anatilia mkazo ushindi walioupata na ule wa vyama vya siasa kali.

"Vyama vya kihafhidina vimeshinda. Lakini ni ukweli pia kwamba vyama vya siasa kali za kushoto na kulia vimeungwa mkono, na ndiyo maana matokeo yanakuja na uwajibikaji mkubwa kwa wahusika katika vyama vyetu. Tunaweza kutofautiana katika mambo binafsi, lakini sote tuna nia ya utulivu, na sote tunataka Ulaya yenye nguvu na yenye ufanisi kwa hivyo katika muda wote wa kampeni yangu, nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii ili kuunda kundi kubwa la vyama vinavyounga mkono Ulaya."

Viongozi wa chama cha AfD wakifurahia ushindiPicha: Jörg Carstensen/dpa/picture alliance

Baada ya wiki kadhaa za uvumi kuhusu ushindi wa kishindo wa vyama vya mrengo mkali wa kulia katika uchaguzi huo, hali hiyo imejidhihirisha wazi kwa matokeo ya kushangaza wa chama cha Ufaransa cha National Rally, chama cha Freedom Party cha Austria na chama mbadala kwa Ujerumani cha AfD. Uwepo wa wajumbe wengi wa siasa kali bungeni kuliko ilivyowahi kushuhudiwa kunamaanisha kuwa sauti zao sasa zitatiliwa maanani. 

Baada ya siku nne za kuhesabu kura za raia takribani milioni 180 katika nchi zote 27, mshangao mkubwa ni huko mjini Paris ambako rais Emmanuel Macron amelazimika kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge kabla ya hata zoezi la kuhesabu kura limalizike. Chama chake cha Renaissance kimepata asilimia 15 na kuangushwa na chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally, kilichojizolea zaidi ya asilimia 30 ya kura.