Vyama vya kizalendo Italia kuapishwa
1 Juni 2018Jana jioni, Rais wa Italia Sergio Mattarella alimpa mamlaka kwa mara ya pili Giuseppe Conte kuunda serikali. Conte, profesa wa sheria alitangaza baraza lake lijalo la mawaziri baada ya kukutana na Mattarella. Kiongozi wa chama kinachopinga wahamiaji nchini Italia cha League, Matteo Salvini ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani, huku kiongozi wa Vuguvugu la Nyota Tano, M5S, Luigi Di Maio akiteuliwa kuwa waziri wa maendeleo ya kiuchumi.
Paolo Savona, mkosoaji mkubwa wa kanda inayotumia sarafu ya Euro pamoja na Ujerumani, ameteuliwa kuwa waziri wa masuala ya Ulaya. Awali Savona aliteuliwa kuwa waziri wa uchumi, lakini Rais Mattarella alikataa kuidhinisha uteuzi wake. Nafasi ya wizara ya uchumi, ambayo itahusika zaidi na masuala ya fedha, imeenda kwa Giovanni Tria, mchumi ambaye anatetea hatua ya kupunguza kodi, lakini anaunga mkono Italia kubakia katika kanda inayotumia sarafu ya Euro.
Enzo Moavero Milanesi ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje. Katika baraza hilo lenye mawaziri 18, wanawake ni watano tu. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Italia, mawaziri hao kutoka vyama vya kizalendo, watapigiwa kura ya kuwa na imani nao katika mabunge yote mawili Jumatatu au Jumanne ijayo.
Pongezi za Rais Mattarella
Baada ya kuundwa kwa serikali hiyo mpya, Mattarella amemshukuru na kumpongeza Conte kwa kazi kubwa aliyoifanya. ''Ningependa kuzungumza maneno machache tu kukushuruku kwa kazi yao kubwa, kwa wakati wote huu, katika safari hii ngumu ya kuunda serikali. Nakutakia mafanikio mema zaidi kwenye majukumu yako katika siku zijazo,'' alisema Mattarella.
Italia imekuwa katika mkwamo wa kisiasa kwa karibu miezi mitatu baada ya uchaguzi wa Machi 4 ambao matokeo yake hayakufanikiwa kumtoa mshindi wa moja kwa moja. Hatua hiyo ilisababisha wasiwasi katika masoko ya fedha pamoja na kuwepo hofu miongoni mwa wanachama wanaotumia sarafu ya Euro ambao ni washirika wa Italia.
Mipango ya serikali mpya inajumuisha kuharakisha zoezi la kuwaondoa wahamiaji haramu na kupambana na biashara ya kuuza watu. Pia muungano huo umeahidi kuchukua hatua kadhaa katika Umoja wa Ulaya ikiwemo kufanya tena mazungumzo kuhusu mikataba ya umoja huo na kupitia upya masuala ya utawala wa kiuchumi ya umoja huo kama vile sarafu moja.
Hata hivyo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, ameonya kuhusu kuutupia lawama umoja huo kutokana na matatizo yote ya Italia. Juncker amesema wanaipenda Italia, lakini hawezi kukubali kubeba lawama kwamba umoja huo haukufanya jitihada za kuyatatua matatizo ya Italia.
Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia nchini Ufaransa, National Front, Marine Le Pen amempongeza Salvini kwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya muungano. Ameuita muungano huo kama 'ushindi wa demokrasia dhidi ya vitisho vya Umoja wa Ulaya''. Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Le Pen amesema hakuna jambo litakalowazuia watu kurejea katika hatua ya kihistoria.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Abudl-Rahman