1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel afikia makubaliano na SPD kuunda serikali ya mseto

Yusra Buwayhid
7 Februari 2018

Vyama vya kihafidhina wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na kile cha Social Democratic (SPD) vimekubaliana juu ya mpango wa kuunda serikali ya pamoja, pamoja na nafasi za mawaziri mbalimbali.

Koalitionsverhandlungen von Union und SPD Merkel Abfahrt
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Vyama vya Ujerumani vilivyopo katika mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto vimeweza kuafikiana juu ya nafasi mbalimbali za mawaziri, lakini bado vinaendelea na mazungumzo kupata makubaliano ya mwisho.

Kulingana na shirika la habari la dpa pamoja na gazeti la Ujerumani la Bild, chama cha SPD kitachukua wizara tatu za juu - wizara ya mambo ya nje, wizara ya fedha na wizara ya ajira na ustawi wa jamii katika serikali mpya ya mseto ya Ujerumani. Wakati chama cha Merkel cha Christian Democratic Union (CDU) kitachukua wizara ya uchumi pamoja na ya ulinzi.

Gazeti la Bild, ambalo halikutaja chanzo cha taarifa yake, limesema mshirika wa Merkel wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer - mwenye misimamo mikali juu ya suala la uhamiaji - atakuwa waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani.

Makubaliano hayo iwapo yatathibitishwa, itakuwa ni hatua moja mbele katika kupatikana serikali nchini Ujerumani baada zaidi ya miezi minne  ya kukosekana kwa uhakika wa kisiasa nchini humo, hali iliodhoodfisha nafasi ya Ujerumani katika masuala ya kimataifa na kuzua mjadala juu ya muda gani Merkel atabaki katika wadhifa huo wa ukansela.

Wanachama wa SPD kupigia kura mpango wa kuunda serikali na Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa na kiongozi wa chama cha SPD Martin SchulzPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Hata hivyo, mpango wowote utakaofikiwa utahitaji kuidhinishwa na wanachama 464,000 wa chama cha SPD, ambao watalazimika kuuidhinisha kwa kura ya posta kabla ya chama hicho kuchukua hatua ya kuunda muungano mwengine tena na vyama vya Merkel baada ya kuwa mshirika wake mdogo tokea mwaka 2013.

Hata hivyo duru nyingine haikuweza kuthibitisha kwamba makubaliano yamefikiwa , na kusema kwamba vyama hivyo bado vinahitaji kusuluhisha masuala kadhaa baina yao.

Mazungumzo hayo yalisongezwa mbele Jumapili iliyopita ambayo ilikuwa iwe siku ya mwisho baada ya kukosekana makubaliano juu ya masuala ya afya na soko la ajira pamoja na ugawanaji wa wizara.

Wanachama wa SPD watapaswa kupiga kura ya kukubali au kukataa makubaliano hayo. Matokeo ya kura hiyo ya maoni yanatarajiwa kuwa tayari mwishoni mwa juma la kwanza la mwezi wa Machi.

Baada ya hapo Merkel atakuwa na mamlaka ya kuteua baraza la mawaziri na vyama hivyo vitasaini mkataba wa serikali ya muungano. Na mambo yote yakienda kama yalivyopangwa, Ujerumani itapata serikali mpya ifikapo mwezi Aprili - ikiwa ni miezi sita baada ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dw/dpa/rtre/

Mhariri: Iddi Sessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW