1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vyaungana dhidi ya Zuma

12 Aprili 2017

Vyama hasimu vya kisiasa nchini Afrika Kusini vimeungana hivi leo kwenye maandamano katika mji mkuu Pretoria wakimshinikiza Rais Jacob Zuma kuondoka madarakani.

South Africa Zuma Challenge
Picha: picture alliance/AP Photo/D.Farrell

Wafuasi wa chama cha mrengo mkali wa kushoto, Economic Freedom Fighters (EFF), wale wa chama kikuu cha upinzani - Democratic Alliance (DA), sambamba na wa vyama vingine vidogo vidogo walikusanyika pamoja kwenye maandamano hayo ya Jumatano, ambayo polisi walisema yalianza kwa amani.

Maandamano hayo kuelekea kwenye eneo la Union Buildings, yalipo makao makuu ya serikali, yameandaliwa katika siku ambayo kiongozi huyo anasherehekea miaka 75 ya kuzaliwa kwake na yanafanyika baada ya maandamano makubwa nchi nzima kumtaka ajiuzulu wiki iliyopita.

Hatua yake ya hivi karibuni kumfukuza waziri wa fedha anayeheshimiwa sana, Pravin Gordhan, imemfanya apoteze uungwaji mkono wa umma huku hasira dhidi ya ufisadi serikalini zikipanda, ukosefu wa ajira ukiwa wa kiwango cha juu na uchumi ukidorora.

Kufukuzwa kwa Gordhan kumemfanya Zuma akosolewe na hata watu wake wa karibu ndani ya chama tawala cha African National Congress (ANC), akiwemo Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa.

"Nimekuja kwa sababu Zuma lazima aondoke madarakani. Aliiuza nchi hii. Simtaki tena," Mavis Madisha (37), mfuasi wa EFF, aliliambia shirika la habari la AFP. 

Waafrika Kusini wakusanyika tena kumpinga Rais Jacob Zuma wakimtaka ajiuzulu.Picha: Reuters/S.Sibeko

Hata hivyo, ANC imekuwa ikijaribu kuonesha kuungana na Zuma na kuapa kuishinda kura ya kutokuwa na imani dhidi yake bungeni inayotazamiwa kupigwa Jumanne ijayo. 

"Katika wakati huu wa mzozo, sisi, kama vyama vya kisiasa, tunaweka kando tafauti zetu kwa lengo la pamoja - kuiokoa Afrika Kusini kutoka mikononi mwa Jacob Zuma," alisema John Moodey, kiongozi wa DA katika jimbo la Gauteng linalojumuisha pia miji ya Pretoria na Johannesburg.

"Wafuasi wa Zuma watatumia kila mbinu kusalia madarakani, hata kuwatisha wabunge. Lakini kwa kura ya siri tunaweza kumng'oa Zuma kwa wingi mkubwa. Kama haikufanikiwa, basi nakuhakikishia tutakuwa na serikali ya mseto mwaka 2019," aliongeza Moodey.
 
Zuma, aliyeingia madarakani mwaka 2009, anatazamiwa kustaafu kwenye nafasi ya ukuu wa ANC mwezi Disemba na pia kama rais kuelekea uchaguzi wa mwaka 2019. Mwenyewe anaonekana kumpendelea mke wake wa zamani, mkuu wa zamani wa Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, arithi nafasi yake. 

Waandamanaji walibeba mabango yanayosomeka "Zuma lazima aondoke", "Hamba tsotsi" ("Ondoka mwizi"), na "Zuma muongo".

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW