1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi

4 Mei 2015

Vyombo vya habari pamoja na wanasiasa barani Afrika kwa jumla wamenyamaza kimya juu ya maafa ya wakimbizi kwenye bahari ya Mediterania..

Migration Europa Flüchtlinge Mittelmeer
Picha: picture-alliance/dpa/Lupi

Gazeti la wasomi nchini Afrika Kusini "Daily Maverick" limeandika katika makala yake kwamba ni jambo la kushangaza kuona jinsi vyombo vya habari barani Afrika vinavyojikunyata kuhusu suala la maalfu ya wakimbizi wa Afrika wanaostahabu safari za hatari kubwa ili kufika Ulaya. Gazeti hilo limetoa mwito peke yake kutanabahisha kwamba maafa ya wakimbizi kwenye bahari ya Mediterania siyo tatizo la bara la Ulaya peke yake.

Gazeti hilo la Afrika Kusini limetilia maanani katika makala yake kuwa Idara ya mawasiliano ya Umoja wa Afrika ilitingwa na uchaguzi wa rais nchini Sudan.

Idara hiyo ilipaswa itoe tamko juu ya uchaguzi huo, tamko juu ya Wakristo wa Ethiopia waliouliwa na magaidi wa linaloitwa dola la kiislamu na pia ilipaswa kutoa tamko juu ya matukio ya nchini Afrika Kusini ambako wageni walishambuliwa .

Gazeti la " Daily Maverick" limesema idara ya mawasiliano ya Umoja wa Afrika iliweza kuinadi Afrika kwa lengo la kuvutia vitega uchumi ili kuhimiza "ajenda ya Afrika ya mwaka 2063" lakini gazeti hilo limeeleza kwamba idara ya mawasiliano ya Umoja wa Afrika haikulizingatia suala la wakimbizi wa Afrika wanaostahabu safari za hatari katika mashua ili kufika barani Ulaya.

Mkuu wa idhaa ya Afrika Claus Staecker.

Siyo raha na starehe tu

Hata hivyo Umoja wa Afrika umesema kuwa unajaribu kuwafanya wakimbizi kutoka bara hilo waelewe, wangali wakiwapo kwenye kambi ,kwamba kinachowasubiri barani Ulaya siyo raha na starehe tu .Hiyo ni hatua nzuri ya kwanza lakini hakuna jingine zaidi ya hapo.

Magazeti kadhaa ya Afrika yamesisitiza hayo ikiwa pamoja na "Johannesburg Star" "Pretoria News" au gazeti la "New Vision" kutoka mji mkuu wa Uganda Kampala. Gazeti hilo linapiga vijembe kwa kusema Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua hatua .

Gazeti la nchini Senegal "Sud Quotidien" limejaribu kukiangalia kiini cha tatizo la wakimbizi-vichwa vya habari vya gazeti hilo vinasema,"jihad,Barcelona au kifo" Hayo yanafichua mengi: yaani mradi mtu aondoke bila ya kujali kile kitakachotokea.

Ulaya inastahili kulaumiwa

Gazeti la Zimbabwe "Zimbabwe Times" linalochapishwa nje ya nchi linazilaumu, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kwa kushindwa kuchukua hatua.Gazeti hilo linasema Umoja wa Ulaya unasuasua kuchukua hatua za kuwalinda vijana wa Afrika dhidi ya wahalifu wanaowasafirisha watu kinyume na sheria.

Gazeti la "The Observer" linatilia maanani kwamba hakuna msimamo wa pamoja miongoni mwa nchi za Afrika juu ya suala la wakimbizi. Na linasema hali halisi inawafanya watu waulize iwapo viongozi wa Afrika wanao uwezo wa kuielekeza historia ya Afrika katika mkondo sahihi ili Waafrika wasichekwe!

Mwandishi: Stäcker Claus.

Mfasiri:Mtullya abdu

Mhariri:Gakuba Daniel