1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyombo vya habari Tanzania vyatakiwa kupinga rushwa ya ngono

9 Februari 2021

Vyombo vya habari Tanzania vimetakiwa kuwa na sera ndogo ya kupinga rushwa ya ngono katika vyumba vya habari inayoonekana kushamiri katika kipindi cha hivi karibuni hasa kwa waandishi waolipwa kwa kila taarifa au makala.

Hawa Bihoga  Edda Sanga
Picha: Tamwa

Katika utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA ukihusiana na hali ya rushwa ya ngono katika vyombo vya habari umebaini suala la rushwa ya ngono katika sekta hiyo inaendelea kushamiri huku wanaoathirika zaidi ni waandishi habari wanaolipwa kwa ripoti au makala wanazoandika, wale wanaojitolea ili kupata ujuzi pamoja na wanafunzi wanaofanya masomo kwa vitendo.

Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza

Matokeo ya utafiti mdogo uliofanywa kwa mkoa wa Dar es Salaam pekee ambao ndio umebeba asilimia kubwa ya vyombo vya habari vya kitaifa, umeonesha kati ya waliohojiwa asilimia 48 wameoneshwa wamewahi kukumbwa na kadhia ya rushwa ya ngono huku asilimia 52 hawakutaka kabisa kuzungumza chochote juu ya suala hilo ambalo ni jinai kwa mujibu wa sheria ya rushwa ya ngono ya mwaka 2007 nchini humo.

Rose Ruben mkurugenzi mtendaji wa TAMWA amewaambia waandishi habari kuwa kulingana na hali ilivyo kuna haja ya kuwa na sera ndogo itakayodhibiti rushwa ya ngono katika vyumba vya habari ikiambatana na ukumbusho wa mara kwa mara juu ya suala hilo.

Waandishi habari wanawake wakiwa katika moja ya mikutanoPicha: DW/V. Natalis

Sehemu ya utafiti inaonesha suala la rushwa ya ngono wanaelewa, lakini waandishi wanawake ndio waathirika wakubwa juu ya kadhia hiyo huku wengi kati yao wakishindwa kuzungumza katika vyombo vya kisheria wakihofia kupoteza ajira zao, kupata aibu sehemu za kazi kadhalika kutokuwa na madawati ya jinsia katika vyumba vya habari.

Wadau walioshiriki katika utafiti hupo mdogo wanaainisha kuwa sababu ya kushamiri kwa rushwa ya ngono ni kutokana na baadhi ya waandishi kutojiamini kwenye utendaji kazi, kujirahisisha wenyewe, hali kadhalika kutokuwa washindani hivyo kushindwa kufurukuta wanapokumbwa na vitendo vya rushwa ya ngono, kama alivyofafanua Neema Kasabulilo, afisa habari na utafiti kutoka taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa Afrika MISA-TAN.

Kutokana na utafiti huo jeshi la polisi kupitia Mrakibu Mwandamizi wa jeshi hilo dawati la jinsia kanda maalum Leah Mbunda anatoa wito kwa waandishi habari kuhakikisha wanavunja ukimwa linapokuja suala la rushwa ya namna yoyote kwani ni kinyume cha utamaduni, maadili na sheria za Tanzania.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW