Vyombo vya habari vya Tanzania viliegemea chama tawala
14 Desemba 2021Ripoti hiyo ilibaini kuwa vyombo vya habari havikuweza kutekeleza ipasavyo wajibu wa kimsingi wa kuripoti uchaguzi huo, ambapo vyombo vya habari vilitoa zaidi nafasi kwa chama cha mapinduzi kuliko kwa vyama upinzani, huku vyombo vya habari vya habari vya serikali vikionekana kutoa taarifa zaidi za mgombea wa CCM ukilinganisha na vyama vingine.
Kiongozi Mkuu wa utafiti huo, Dk Abdallah Katunzi anasema hali haikuwa nzuru na kadhalika ilikuwa mbaya zaidi kwa vyombo vinavyomilikiwa na serikali, ukilinganisha na vyama vingine vya upinzani.
Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa vyombo vingi vya habari vilijikita katika kuripoti habari za wagombea huku wananchi hasa wanawake wakikosa nafasi nzuri katika ripoti hizo licha ya takwimu kuonyesha Tanzania ina idadi kubwa ya wanawake. Katunzi hapa anaeleza sababu za mapungufu hayo katika kuripoti habari za uchaguzi.
Waziri Mkuu wa Zamani wa Tanzania Jaji Joseph Sinde Warioba ataka marekebisho katika sekta ya habari.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema tunahitaji kufanyia kazi mapungufu yaliyoorodheshwa katika ripoti hiyo kwa kuvipa uhuru vyombo vya habari. Amesema Tanzania imefika mahali vyombo vya habari vinaogopa kuripoti hitilafu zilizojitokeza katika chaguzi hizo.
Jaji Warioba amesema ripoti hiyo itasaidia siku za usoni wakati taifa linaendelea kuimarisha shughuli za vyombo vya habari katika jamii. Akaongeza kuwa kwa sasa habari za rais zinapewa kipaumbele badala ya maoni ya wananchi kuonekana katika habari hizo na hivyo akashauri vyombo vya habari kuendelea kuwafunda wanahabari katika weledi. Jaji Warioba akasema zipo taasisi zenye madaraka ambazo hutoa adhabu kubwa kwa vyombo vya habari.
Ripoti yaonesha wanawake hawajapata nafasi pana katika baadhi ya vyombo vya habari
Ripoti hiyo kadhalika ilionyesha kuwa sauti za wanawake zilisikika katika uchaguzi uliopita ambapo baadhi ya vyombo vya habari vilifanya vizuri kujumuisha sauti za wanawake katika ripoti zao. Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake TAMWA Joyce Shebe anaeleza hapa umuhimu wa sauti za wanawake.
Ripoti hiyo imeonyesha zaidi kuwa vyombo vingi vya habari vilitetereka kutokana na sheria kandamizi na zinazominya uhuru wa habari, kushuka kwa weledi kwa baadhi ya wahariri, hali mbaya ya uchumi, hali ya umiliki wa chombo cha habari na mazingira magumu na yasiyo rafiki ya kisiasa.
Chanzo: DW Dar es Salaam