1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyuo vukuu vya umma nchini Kenya vyakabiliwa na mgomo

19 Septemba 2024

Masomo katika vyuo vikuu vya umma nchini Kenya yamekatizwa kutokana na mgomo wa kitaifa wa wahadhiri wanaoishinikiza serikali yao kuwalipa stahili zao.

Chuo Kikuu cha Nairobi Tarehe 11 Januari 2011.
Chuo Kikuu cha Nairobi Tarehe 11 Januari 2011.Picha: CC BY-SA 3.0 Wing

Wanataka serikali kuu iutekeleze mkataba wa maelewano wa mwaka 2021- 2025 unaoainisha swala la mishahara, marupurupu na bima ya afya. Mgomo huu umeitia joto zaidi sekta ya elimu ambayo imegubikwa na malalamiko kuhusu mfumo wa serikali wa malipo ya karo na ufadhili wa masomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini humo. 

Masaibu katika sekta ya elimu ya juu kwenye vyuo vikuu vya umma nchini Kenya yanaendelea baada ya juhudi za kuzuia mgomo wa kitaifa wa wahadhiri hao kugonga mwamba miungano ya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu ya UASU na KUSU mgomo unaojiri takriban wiki moja tu baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu kusitisha mgomo wao baada ya serikali kuingilia kati.

Wahadhiri wahatarudi darasani hadi muafaka upatikane

Profesa Rayya Timamy kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya Mei 6, 2016 Picha: DW/M. Khelef

Kulingana na wahadhiri wanaoshiriki mgomo huo na wengine wakiwemo kushiriki maandamano, wanazidi kushikilia kuwa, hawatarejea kazini hadi pale serikali itakapotekeleza kikamilifu mkataba wa maelewano wa mwaka 2021 - 2025, sawia na kusawazishwa kuwasilishwa kwa mikato ya mishahara yao katika bima ya afya, kusawazishwa kwa marupurupu yao na nyongeza ya mishahara.

Wanalalamikia pia kucheleweshwa kwa mishahara yao wanayosema inawaweka katika hali ngumu ya kimaisha ikizingatiwa hali ngumu ya kiuchumi anavyoelezea afisa kutoka muungano wa kitaifa wa wafanyikazi hao jimbo la Busia Nicholus Kirinya anasema"Hatupatiwi pesa tunayohitaji kwa kujikimu mahitaji yetu, hatupati kamwe, pesa yenye wanatupatia zingine, SACCO zimekuja wanatupigia mlango kila siku pesa yetu iko wapi ndio tunauliza waangalie hiyo maneno, sisi tunaumia"

Kadhalika, wameelekezea kidole cha lawama tume ya kuratibu mishahara ya wafanyikazi wa umma SRC imewatelekeza wakisema makubaliano ya mwisho waliyojadili na serikali ni ya mwaka 2013 - 2017 na kutoka wakati huo bado na hivyo kutoa wito kwa tume hiyo kutekeleza ushauri kuhusu swala lao.

Himizo la wanafunzi kuwa na subra kwa hali iliyopo

Wamehimiza wanafunzi kuwa na subra wakisisitiza kuwa, lengo lao ni kumalizachangamoto zinazowakabili kwa sasa ili wapate kurejelea majukumu yao ikizingatiwa mgomo huu umeathiri vyuo vikuu vya umma 35.

Katibu mkuu wa muungano wa UASU Constatine Wasonga amesema miiungano yote miwili itaendelea na mazungumzo na serikali hadi pale makubaliano stahili yatakapoafikiwa ikisema wana haki sawia na wafanyakazi wengine wa serikali walioongezewa asilimia 10 ya mishahara yao" Walidhani ni mzaha, na haturudi nyuma, nimeona barua inasambazwa ikisema makansela wa vyuo wanasema tumekubaliana kuhusu mkopo wa magari na nyumba, nio tumekubaliana ni asilimia 3 ila hatujaambiwa ni kiasi gani serikali imetenga kwa gari na nyumba."

Soma zaidi:Ujerumani na Kenya zasaini mkataba wa uhamiaji na ajira

Haya yanajiri huku viongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi wakisuta hatua ya kubuniwa kwa jopo kazi la kuangazia mfumo mpya wa kuwafadhili wanafunzi wa taasisi za elimu  ya juu wakisisitiza hawataki ufanyiwe marekebisho yanayopendekezwa wakilaumu mfumo huo kuchangia baadhi ya wanafunzi kukatiza masomo yao na wengine kukosa kujiunga na vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu.  Wametoa ilani ya siku 14 kushiriki maandamano.

 

DW Kusumu