1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafghani waandamana kupinga uingiliaji wa Pakistan

Admin.WagnerD7 Septemba 2021

Wakati kundi la Taliban likiwa linadai ushindi katika mapigano ya Panjshir, baadhi ya Waafghani wamekuwa wakiandamana kupinga kile kinachodaiwa kuwa ni uingiliaji kati wa Pakistan katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Afghanistan Kabul Demonstration gegen Pakistan
Picha: HOSHANG HASHIMI/AFP

Wapiganaji wa Taliban wamefyatua risasi angani Jumanne katika mji mkuu wa Kabul, kuyatawanya makundi ya watu waliokuwa wamekusanyika kwa maandamano ya kupinga uingiliaji kati wa serikali ya Pakistan nchini mwao.

Watu wasiopungua 70, wengi wao wakiwa wanawake, walijitokeza nje ya ubalozi wa Pakistan, wakishikilia mabango huku wakiimba dhidi ya kile walichosema uingiliaji kati wa Pakistan, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikituhumiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Taliban.

Soma zaidi:Vita vyapamba moto Panjshir kati ya Taliban na waasi

Wakati Taliban ikiwa bado inasubiriwa kutangaza serikali, wananchi wa Afghanistan wanaohofia kujirudia kwa utawala wa kikatili wa kundi hilo ulioshuhudiwa kati ya mwaka 1996 hadi 2001 - wamekuwa wakifanya maandamano ya makundi madogo madogo katika miji tofauti ikiwa ni pamoja na Kabul, Herat na Mazar-i-Sharif.

Aidha kwa wale wanaotaka kuihama nchini hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema wizara yake inashirikiana na Taliban kuhakikisha kuna ndege za kutosha za kuwasafirisha Waafghanistan wanaotaka kuondoka baada ya jeshi la Marekani na ujumbe wake wa kidiplomasia kuiaga nchini hiyo hivi karibuni.

Afghanistan | Taliban kwenye kiti cha gavana huko PanjshirPicha: Social media/REUTERS

"Tumekuwa pia tukishirikiana na Taliban juu ya mada hii. Na hivi punde wamesema kwamba watawaruhusu watu wenye hati za kusafiri kuondoka kwa uhuru, tutahakikisha wanatimiza ahadi hiyo," amesema Blinken.

Uturuki haina haraka kulitambua kundi la Taliban

Blinken ameyasema hayo leo katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari na wanadiplomasia wakuu wa Qatar na maafisa wa ulinzi. Waziri huyo wa Marekani pamoja na Katibu wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin wako Qatar kulishukuru taifa hilo la Kiarabu kwa msaada wake wa kuwasafirisha maelfu ya watu waliotaka kuikimbia Afghanistan baada ya Taliban kuchukua udhibiti wa mji wa Kabul mnamo Agosti 15.

Halikadhalika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema leo kwamba kuongeza usalama katika uwanja wa ndege ndilo suala kuu kwa wakati huu, na kwamba hakuna haraka ya kulitambua kundi la Taliban kama utawala halali wa Afghanistan.

Soma zaidi:Taliban kutangaza serikali ya "mpito" muda wote, yataka kutambuliwa

Ameongeza kwamba serikali mpya ya Afghanistan itahitaji kujumuisha makundi tofauti ya watu katika jamii, huku akisisitiza wanawake na makabila kadhaa wanapaswa kupewa yadiga za uwaziri.

Aidha hapo jana kundi la Taliban kwa upande wake limedai kuwa sasa linaidhibiti Afghanistan yote, baada ya kushinda mapigano muhimu yalokuwa yakiendelea katika Bonde la Panjshir, ng'ome ya mwisho ya upinzani dhidi ya utawala wao.

Vyanzo: afp, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW