1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Waafghan wanaofukuzwa Pakistan wakabiliwa na madhila makubwa

6 Novemba 2023

Mashirika ya misaada yamesema raia wa Afghanistan wanaoikimbia Pakistan kuepuka kukamatwa na kufukuzwa wanalala nje bila hifadhi stahiki, chakula, maji ya kunywa na vyoo mara baada ya kuvuka mpaka na kuingia nchini mwao.

Afghanistan |Raia wa Afghanistan wanaorudi kwenye kivuko cha mpaka cha Torkham
Muonekano wa jumla unaonyesha wakimbizi wa Afghanistan waliowasili kutoka Pakistani kwenye kambi ya muda karibu na mpaka wa Afghanistan na Pakistan wa Torkham katika jimbo la Nangarhar Novemba 2, 2023. Picha: Wakil KOHSAR/AFP/Getty Images

Pakistan iliitangaza Oktoba 31 kuwa tarehe ya mwisho kwa wahamiaji wa Afghanistan wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria kuondoka au wakabiliwe na kitisho cha kukamata, kama sehemu ya ukandamizaji mpya dhidi ya wahamiaji haramu.

Raia hao wa Afghanistan wanaodoka Pakistan kupitia vivuko viwili  - cha Torkham na Chaman. Utawala wa Taliban unasema umeunda kambi katika upande wa pili wa mpaka kwa ajili ya watu kukaa wakati wakisubiri kuhamishiwa kwenye maeneo yao ya asili nchini Afghanstan.

Soma pia: Wakimbizi 15,000 wa Afghanistan waondoka Pakistan

Mashirka ya misaada yanasema kivuko cha Torkham hakina hifadhi sahihi, hakuna maji ya kunywa, vyanzo ya upashaji joto mbali ya moto wa wazi, hakuna mwanga wala huduma za vyoo.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na ya misaada yanaunda vituo vya mapokezi kwa ajili ya malefu ya watu wanaoingia Afghanistan kila siku.

Kayal Mohammed aliishi katika mji wa kaskazini-magharibi mwa Pakistan wa Peshawar kwa miaka 17. Ana watoto watano na alikufukuzwa hadi mpaka wa Afghanistan karibu wiki moja iliyopita.

Raia wa Afghanistan wakiwa kwenye foleni wakisubiri kuchunguzwa ili kupata msaada wa kibinadamu kwenye kivuko cha mpaka wa Torkham kati ya Pakistan na Afghanistan, Oktoba 30, 2023.Picha: The Norwegian Refugee Council/REUTERS

Aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba hakuruhusiwa kuchukua kitu chochote cha nyumbani kwake.

Binti yake Hawa, mwenye umri wa miaka saba, analia wakati wote kwa sababu ya baridi, akinywa chai kwa kutumia chupa iliyokatwa, huku akilala bila cha kujifunika.

Baba yake ameiomba jumuiya ya kimataifa kuwasaidia. "Hatuwezi kuiomba serikali ya Taliban", alisema. Hawana chochote kwa sababu bado hawajatambuliwa kama serikali, tunaomba kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia hali yetu na kutusaidia nyumba na makazi. Kuna familia ambazo hazina kitu hapa, hazina ardhi, hazina nyumba, zinaishi tu katika uwazi, hakuna anayezisaidia."

Hatari ya ajira kwa watoto

Thamindri Da Silva, kutoka shirika la misaada na maendeleo la World Vision International, alisema watu wengi wanahamishiwa kwenye mto mkavu mara baada ya kupitia usajili wao wa awali na kushughulikiwa katika kituo cha usafiri.

Soma pia:Taliban yaiomba Pakistan kutoa muda zaidi kwa raia kuondoka 

Watu wanaingia Afghanistan wakiwa na nguo zao tu kwa sababu saa zao, vito na pesa vilichukuliwa kwenye mpaka wa Pakistani, aliongeza.

Arshad Malik, mkurugenzi mkazi wa shirila la Save the Children nchini humo, alisema wengi wa wanaorejesa hawana vyeti vyovyote vya elimu, na hivyo kufanya kuwa vigumu kuendelea na masomo yao, na pia hawazungumzi lugha za wenyeji za Dari na Pashto, kwa sababu walisoma Urdu na Kiingereza nchini Pakistan.

Msichana wa Afghanistan akiwa amembeba mdogo wake wa miezi saba Haleema, wakati familia yake ikirejea nyumbani, baada ya Pakistan kutoa onyo la mwisho kwa wahamiaji wasio na vibali kuondoka, nje ya vituo vya urejeshaji vya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) katika mji wa Azakhel huko Nowshera, Pakistan Novemba. 3, 2023.Picha: Fayaz Aziz/REUTERS

Alionya kuwa ajira ya watoto nchini Afghanistan pamoja na ushiriki wao katika magendo huenda vikaongezeka kutokana na umaskini kwani familia nyingi zinazorejea ni miongoni mwa wahamiaji maskini zaidi nchini Pakistan.

"Usafirishaji haramu wa watoto huko Torkham ulikuwa moja ya wasiwasi kutoka zamani, kwa hivyo ushiriki wa watoto katika magendo na usafirishaji wa bidhaa haramu utaongezeka," Malik alisema.

Soma pia:Wakimbizi 10,000 wa Afghanistan wakimbilia mpaka wa Pakistan 

Papa Francis katika hotuba yake ya hadhara Jumapili huko Vatican alikemea hali ya "wakimbizi wa Afghanistan waliopata hifadhi Pakistani lakini sasa hawajui pa kwenda tena."

Changamoto zinazoikabili Afghanistan

Taliban wanasema wana kamati zinazofanya kazi  wakati wote kuwasaidia Waafghanistan kwa kusambaza chakula, maji na blanketi. Afghanistan imelemewa na changamoto zinazochangiwa na kutengwa kwa serikali inayoongozwa na Taliban na jumuiya ya kimataifa.

Miaka ya ukame, uchumi uliodorora na matokeo ya miongo kadhaa ya vita vimesababisha mamilioni ya Waafghanistan kuhama makazi yao.

Wasiwasi umeongezeka miongoni mwa jumuiya ya kibinadamu kuhusu nchi hiyo maskini kutokuwa na uwezo wa kuwasaidia au kuwajumuisha tena raia wake ambao kwa sasa wanalazimishwa kuondoka Pakistan.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW