Waafghanistan waomboleza mauaji ya kikatili
1 Juni 2017Wakati huo huo raia wa nchi hiyo wameendelea na maombolezo ya ndugu zao na marafiki huku wengine wakikesha hospitali kujua hali za majeruhi.
Katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa jana jioni, shambulio hilo limepangwa na mtandao wa wapiganaji wa Haqqan kwa kushirikiana na kurugenzi ya taifa ya usalama ya Pakistan ISI. Mtandao wa Haqqan unatajwa kuwa na wapiganaji katili walio na mashirikiano ya karibu na kundi la Taliban. Afghanistan kwa muda mrefu imeituhumu Pakistan kwa kuyaunga mkono makundi ya Haqqan, wasomi wa Taliban na wapiganaji. Hata hivyo kundi la Taliban limekana kuhusika na shambulio hilo na hakuna kundi lolote hadi sasa lililodai kuhusika.
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani alilaani shambulio hilo akiliita kama "shambulizi la woga lililofanywa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan. "Ninatuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga kufuatia shambulizi la kigaidi la mjini Kabul ambalo limeua na kuwajeruhi ndugu zetu wengi na kuharibu miundombinu ya umma. Kilikuwa ni kitendo cha kinyama ambacho kimesababisha ndugu zetu kujawa na huzuni katika mwezi mtukufu wa Ramadhani," amesema rais Ghani.
Wakati huo huo raia wa Afghanistan wameanza maombolezo ya ndugu zao waliowapoteza katika shambulizi hilo. Wengine wameendelea kusubiri hospitali ili kufahamu hali za ndugu zao waliojeruhiwa. Mshambuliaji aliendesha lori katika eneo lenye ulinzi wa hali ya juu katika ofisi mbalimbali za balozi na majengo ya serikali majira ya asubuhi, na kusababisha uharibifu mkubwa na tafrani. Majeruhi wengi ni raia wakiwemo wanawake na watoto lakini pia mauaji hayo yamehusisha maafisa wa usalama wa Afghanistan.
Viongozi mbalimbali duniani wamelaani vikali shambulizi hilo. Stephane Dujaric ni msemaji wa Umoja wa Mataifa na anasema "Katibu Mkuu amechukizwa na kitendo hiki na kusisitiza haja ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugaidi na vikundi vyenye misimamo mikali. Mauaji ya kiholela ya raia ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za binadamu na hayawezi kuhalalishwa. Wote waliohusika na shambulizi hili lazima wachukuliwe hatua za kisheria."
Mabomu yalikuwa yamefichwa katika tangi la gari iliyokuwa ikitumika kusafisha mfumo wa maji taka, kwa mujibu wa kaimu msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Najib Danish. Malori hayo hutumika mara kwa mara katika mji wa Kabul wenye wakazi karibu milioni 4 ambao hauna mfumo mzuri wa maji taka na kutegemea magari ya kunyonya taka hizo huku mifereji ya maji taka mara nyingi ikiwa wazi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DPA/AP
Mhariri: Josephat Charo