1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafrika Kusini wanapiga kura katika uchaguzi mkuu

8 Mei 2019

Wananchi wa Afrika Kusini leo wanapiga kura katika uchaguzi wa rais na wabunge, ambao chama tawala cha African National Congress, ANC kinapewa nafasi kubwa ya kushinda.

Südafrika Wahlen Mmusi Maimane in Soweto
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Wananchi wa Afrika Kusini leo wanapiga kura katika uchaguzi wa rais na wabunge, ambao chama tawala cha African National Congress, ANC kinapewa nafasi kubwa ya kushinda, licha ya kuwepo kashfa za rushwa, kusuasua kwa uchumi na ukosefu wa ajira.

Chama cha ANC ambacho kimekuwepo madarakani tangu mwaka 1994, kilishinda katika chaguzi zote tano zilizopita na kinapewa nafasi ya kushinda tena, ingawa sio kwa  kura nyingi na licha ya kuwepo kashfa za rushwa, kusuasua kwa uchumi na ukosefu wa ajira.

Hata hivyo, uchaguzi huo utakuwa mtihani mkubwa iwapo kiongozi wake Rais Cyril Ramaphosa atafanikiwa kuyabadili mawazo ya wapiga kura wa Afrika Kusini ambao hawaridhiki na hali ya mambo ilivyo nchini mwao.

Rais wa Afrika Kusini na mwenyekiti wa ANC, Cyril Ramaphosa Picha: Getty Images/AFP/M. Spatari

Uchaguzi huu unafanyika ikiwa ni miaka 25 baada ya Nelson Mandela kukiingiza madarakani chama cha ANC, katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliohitimisha utawala wa ubaguzi wa rangi. Uungwaji mkono wa ANC umekuwa ukipungua katika kila uchaguzi tangu mwaka 2004, ambapo chama kilishinda kwa asilimia 54 ya kura mwaka 2016 katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ikilinganishwa na asilimia 62 katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2014.

Huku vyama 47 vya upinzani vikishiriki katika uchaguzi huo mkuu, vyama pekee vikuu vya upinzani vya Democratic Alliance, DA chenye msimamo wa kati na Economic Freedom Fighters, EFF cha mrengo mkali wa kushoto, ndivyo muhimu zaidi. Kiongozi wa chama cha DA, Mmusi Maimane anagombea kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu tangu alipochukua uongozi wa chama mwaka 2015.

Democratic Alliance kupata asilimia zaidi

Chama hicho kinatarajiwa kupata asilimia zaidi ya zile kilichopata katika uchaguzi wa mwaka 2014, ambazo ni 22. Akizungumza baada ya kupiga kura mjini Soweto, Maimane amesema ni muhimu kupiga kura katika eneo hilo kwenye uchaguzi huo wa kihistoria ili kuelezea matumaini na mustakabali wa nchi yao.

Kiongozi wa EFF Julius MalemaPicha: picture-alliance/M. Safodien

''Kwangu mimi Soweto inaniwakilisha kwa njia nyingi sana, ni nyumbani ambako kuna mapambano na sasa tunaingia katika mapambano mapya, mapambano ya ajira kwa Waafrika Kusini wengi na hivyo ninawasihi watu wa nchi hii kujitokeza kwa idadi kubwa leo,'' alisema Maimane.

Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 66 alichukua madaraka mwaka uliopita kutoka kwa Jacob Zuma aliyelazimishwa kujiuzulu kuwa mwenyekiti wa ANC, baada ya kukiongoza kwa miaka tisa na kukabiliwa na madai ya rushwa na matatizo ya kiuchumi. Utafiti wa maoni unaonesha kuwa chama cha ANC kitajinyakulia karibu asilimia 60 ya kura katika uchaguzi wa leo.

ANC imekuwa ikikosolewa kwa kushindwa kupambana na tatizo la umaskini na kukosekana kwa usawa baada ya enzi za utawala wa kibaguzi. Mwalimu kutoka Coligny, kaskazini magharibi mwa Afrika Kusini, Lockie Mans anasema wananchi hawana furaha na ANC, lakini bado wanaendelea kuichagua.

Uchumi wa Afrika Kusini ulikua kwa asilimia 0.8 mwaka 2018 na kiwango cha ukosefu wa ajira kimeongezeka kwa kiasi ya asilimia 27, huku zaidi ya asilimia 50 ya wasio na kazi wakiwa ni vijana.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW