Waafrika Kusini wapiga kura kulichagua bunge jipya
29 Mei 2024Uchaguzi huo unaonekana kama ndio muhimu zaidi tangu mpigania uhuru na kisha baadae rais Nelson Mandela alipoiongoza nchi hiyo kupata demokrasia mwaka wa 1994.
Soma pia: Raia nchini Afrika Kusini waanza kupiga kura ya mapema
Chama cha African National Congress - ANC, ambacho kimetawala Afrika Kusini mfululizo tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi, kipo katika hatari ya kupoteza wingi wake wa viti bungeni kwa mara ya kwanza tangu wakati huo. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, ANC inatarajiwa kupata chini ya asilimia 50 ya kura na itahitajika kuunda serikali ya muungano.
Afrika Kusini inakabiliwa na uchumi unaodhoofika, ukosefu mkubwa wa ajira na umaskini, kukatika kwa umeme mara kwa mara, na huduma mbovu za usambazaji maji, mfumo unaoporomoka wa huduma za afya pamoja na viwango vya juu vya uhalifu na mfumo wa haki ya jinai usiofanya kazi. Wanachama wa vyama 52 wanashindania viti 400 katika bunge la kitaifa.
Soma pia: Democratic Alliance yawataka Waafrika Kusini kuiangusha ANC
Serikali mpya za mikoa pia zitachaguliwa. Kati ya watu milioni 40.1 wenye uwezo wa kupiga kura, ni milioni 27.4 ambao wamesajiliwa kupiga kura. Bunge jipya litakalochaguliwa lazima kisha liunde serikali na kumchagua rais katika kipindi cha siku 14.