1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafrika Kusini wako vituoni kuchagua serikali za mitaa

1 Novemba 2021

Wapiga kura wadaiwa kuchoshwa na chama cha ANC kutokana na matatizo mengi yanayowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa huduma muhimu ambazo ni maji na umeme

Südafrika Pretoria | Amtseinführung Cyril Ramaphosa, Präsident
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Waafrika Kusini wanapiga kura kuchagua serikali za mitaa katika uchaguzi wa manispaa ambao unatarajiwa kutoa sura ya namna walivyochoshwa na kutoridhika na chama  kilichoko madarakani cha African National Congress ANC.

Chama tawala African National Congress kimepoteza umaarufu siku nyingi hata kabla ya machafuko yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu yaliyoshuhudiwa mwezi Julai mwaka huu baada ya kutiwa jela aliyekuwa rais wa nchi hiyo bwana Jacob Zuma.

Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Uchunguzi wa maoni ya wapiga kura unaonesha kwamba wapiga kura wengi huenda kwa mara ya kwanza wakakipa kisogo chama hicho ambacho kimeitawala nchi tangu ulipoondolewa utawala wa wazungu mnamo mwaka 1994 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza rais mweusi Nelson Mandela.

Kuna changamoto chungunzima zinazoelezwa kuwa sababu ya wapiga kura wengi kutoridhishwa na ANC. Mpiga kura Samule Mahlaule umri wake miaka 55 dereva wa teksi ya Uber na baba wa watoto wanne huko Soweto anasema serikali ya wakati wa utawala ubaguzi wa rangi ilikuwa mbaya lakini alau huduma zilikuweko nchini Afrika Kusini kwa wananchi.

Wakati akitowa maoni hayo alikuwa kwenye msururu wa watu chini ya 20 tu waliokuwa wakisubiri kupiga kura hii leo katika kituo kilichoko karibu na nyumbani alikokulia rais Cyril Ramaphosa. Anasema toka mwaka 1994 anapiga kura lakini safari hii anataka mabadiliko na chama cha ANC hakiwezi kuyaleta mabadiliko hayo.

Katika kitongoji cha  Danville huko Pretoria ambako wakaazi wake wengi ni wazungu wenye maisha ya kipato cha kati mpiga kura Charmaine Barnard mwenye umri wa miaka 57 naye pia analilia mabadiliko anasema sababu kubwa inayomfanya apige kura ni kuleta mabadiliko na kuboresha maisha ya kila mwananchi.

Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe

Kiwango cha watu wasiokuwa na ajira kimefikia asilimia 34.4. Katika machafuko ya mwezi Julai baada ya Zuma kufungwa watu 354 waliuwawa,vurugu, uporaji na uharibifu mkubwa ulishuhudiwa katika nchi hiyo. Lakini kwa wapiga kura wengi matatizo ya kila siku ndicho hasa wanachokilalamikia. Miongo kadhaa ya uongozi mbaya imezifisidi mali za serikali, na kusababisha matatizo chungunzima, mgao wa maji, umeme kukatika mara kwa mara na kutatiza mpaka shughuli zao wenyewe ANC za kampeini. 

Kiasi watu milioni 26 wameandikisha kupiga kura kati ya idadi ya watu kiasi milioni 40 wenye vigezo vya kupiga kura. Katika uchaguzi huo wa manispaa wapiga kura watawachagua madiwani 257. Rais Ramaphosa na viongozi wengine kutoka ANC walizunguuka nchi nzima kufanya Kampeini akiwashawishi wapiga kura kwamba anakisafisha chama hicho.

Na kama ilivyo kwenye chaguzi zote za Afrika Kusini wanajeshi 10,000 wamemwagwa maeneo mbali mbali kuwasaidia polisi kuweka utulivu.Matokeo ya uchaguzi huu ndiyo yatakayotuonesha sura ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2024 itakavyokuwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW