1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji 15 wauwawa na vikosi vya usalama Sudan

18 Novemba 2021

Vikosi vya usalama nchini Sudan wamewauwa waandamanaji 15 na kuwajeruhi wengine kadhaa baada ya kutumia risasi za moto kuyakabili makundi ya watu waliokusanyika kupinga hatua ya jeshi kunyakua madaraka.

Sudan Khartum | Proteste gegen Militärregierung
Picha: AFP/Getty Images

Duru kutoka nchini Sudan zinasema waandamanaji wote 15 waliouwawa ni kutoka wilaya za kaskazini mwa mji mkuu Khartoum, ambazo zimeshuhudia ghadhabu kubwa ya umma unaopinga utawala wa kijeshi.

Muungano wa madaktari nchini Sudan umesema vifo hivyo vinafanya idadi ya waliouwawa tangu kuzuka wimbi la kupinga utawala wa kijeshi kufikia watu 39.

Muungano huo  umesema wengi ya waliopoteza maisha jana walikuwa na majeraha ya risasi kwenye shingo au viungo vingine vya mwili.

Madai ya kutumika risasi za moto yameelezwa pia na waandamanaji wenyewe ikiwemo mmoja aliyetambulishwa na shirika la habari la AFP kwa jina la Soha aliyesema ameshuhudia kwa macho yake mwenyewe mtu akipigwa risasi na polisi mjini Khartoum.

Hata hivyo polisi imepinga kwa matamshi makali madai ya kutumia risasi za moto kuwakabili waandamanaji.

Vifo vya watu 15 ni doa jingine kubwa kwa utawala wa kijeshi 

Makabiliano hayo ya siku ya Jumatano kati ya polisi na waandamanaji ndiyo mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu maafisa wa jeshi walipojitwalia madaraka kupitia mapinduzi ya mnamo Oktoba 25.

Waandamanaji wameapa kutoondoka mitaani Picha: AFP/Getty Images

Licha ya vikosi vya usalama kutumia nguvu waandamanaji wameendelea kupiga kambi kwenye maeneo kadhaa ya mji wa Khartoum na wameapa hawatoondoka mitaani hadi jeshi likabidhi madaraka kwa raia.

Mmoja ya waandamanaji aliyejitambulisha kwa majina ya Ahmed Mahjoub amesema, "Wajibu wa jeshi ni kusimamia usalama, na inapokuja uendeshaji wa serikali, hilo ni jukumu la raia, na dunia nzima ina msimamo mmoja kuhusu hilo"

Kwa upande wake Asasi ya Wanazuoni nchini Sudan inayoratibu maandamano ya kulipinga jeshi nayo pia imesema mauaji ya waandamanaji kimsingi yamezidisha ari ya kuukataa kinagaubaga utawala wa majenerali.

"Siku hii ya mauaji ya halaiki inaongeza uzito wa kaulimbinu yetu: hakuna majadiliano, hakuna ushirikiano wala hakuna kusalimu amri mbele ya jeshi" imesema sehemu ya taarifa ya Jumuiya hiyo iliyotolewa jana jioni.

Juhudi za kidiplomasia zaambulia patupu 

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Baraza la Kijeshi nchini SudanPicha: /AP/dpa/picture alliance

Maandamano ya jana Jumatano yalifanyika licha ya serikali kuzima huduma za simu na intaneti na kutanua kampeni yake ya kuwakamata wanaharakati, waandishi habari na wakati mwingine hata wapita njia.

Juhudi za kimataifa zingali zinaendelea kuwashawishi majenerali kuirejesha madarakani serikali ya mpito ya kiraia. Naibi Waziri

wa mambo ya kigeni wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Molly Phee amekuwa akiongoza kazi ya kutafuta suluhu ya mzozo huo kwa kuzungumza na wanajeshi na viongozi  wa kiraia wa serikali iliypinduliwa.

Lakini licha ya shinikizo la kimataifa, watawala wa kijeshi wa Sudan yumkini wametia pamba masikioni, kwa sababu kwa jumla bado hakuna ishara ya kurejea kwa utawala wa kiraia mjini Khartoum hivi karibuni.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW