1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji Hong Kong watishia kuzingira ofisi za utawala

2 Oktoba 2014

Mamia ya wanafunzi wamefunga njia zinazotoka katika ofisi ya afisa mkuu wa Utawala wa Hong Kong leo, ikiwa sehemu ya maandamano ya wanaharakati wanaotaka demokrasia zaidi katika kisiwa hicho ambacho ni sehemu ya China.

Wanafunzi wameapa kuzitatiza shughuli za serikali ikiwa matakwa yao yatapuuzwa
Wanafunzi wameapa kuzitatiza shughuli za serikali ikiwa matakwa yao yatapuuzwaPicha: Getty Images/P. Bronstein

Hadi alfajiri ya leo wanafunzi kwa mamia walikuwa wamepiga kambi kwenye njia ya kutoka kwenyew ofisi ya Leung Chun-Ying, mwendo wa dakika tano kutoka kituo kikuu cha maandamano ambako maelfu wengine wamejazana katika barabara kuu za Hong Kong. Viongozi wa wanafunzi hao wamesema ikiwa Leung hatajiuzulu leo kama wanavyomtaka kufanya, basi watasimamisha shughuli zote katika kisiwa hicho kwa kuyazingira majengo muhimu ya serikali.

Maandamano ya usiku wa kuamkia leo hayakuwa na vurugu zozote, polisi katika jimbo hilo la China lenye mamlaka ya ndani, wamejizuia kuingilia kati. Kiongozi wa shirikisho la vyama vya wanafunzi Alex Chow, amesema njia hiyo waliyoizuia ni muhimu kimkakati, kwani itazuia uwezekano wa polisi kutumiwa vikosi vya ziada. Kiongozi mwingine wa wanafunzi hao, Agnes Chow, amesema afisa mkuu wa utawala wa Hong Kong hana budi kutoka mafichoni na kujibu maswali ya waandamanaji.

Lakini Leung Chun-Ying amepuuza mashariti hayo ya waandamanaji na amewataka kutawanyika. Serikali mjini Beijing imesimama naye bega kwa bega, na gazeti la chama cha kikomunisti ambalo huwakilisha msimamo wa serikali, limesema kuwa China ina imani kamili kwa kiongozi huyo na inaridhishwa na ufanisi wake.

Leung Chun-Ying, afisa mkuu wa utawala wa Hong Kong amepuuza wito wa kumtaka ajiuzuluPicha: Alex Ogle/AFP/Getty Images

Mzozo wachukua sura ya kimataifa

Mzozo huo wa Hong Kong umekuwa suala muhimu katika mazungumzo kati wa waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Wang Yi ambaye yuko ziarani nchini Marekani, na mwenzake wa Marekani John Kerry. John Kerry amesema Marekani inaunga mkono haki ya Hong Kong kujichagulia viongozi.

''Kama China inavyofahamu tunaunga mkono haki ya Hong Kong kuchagua viongozi wake chini ya mwongozo wa sheria iliyopo, na tunaamini kwamba hali hiyo ni mwafaka kwa ustawi wake. Tunayo matumaini makubwa kuwa mamlaka ya Hong Kong itakuwa na stahamala na kuwaruhusu waandamanaji kueleza mawazo yao kwa amani''. Amesema Kerry.

Akijibu kauli hiyo ya Kery, waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi amesema nchi yake inauchukulia mzozo wa Hong Kong kuwa mambo yake ya ndani, na kuzitaka nchi nyingine kulitambua hilo.

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa China, Wang Yi (kulia) asema mzozo wa Hong Kong ni Mambo ya ndani ya China. Kushoto ni mwenzake wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Wang amesema, ''Uhuru wa China unapaswa kuheshimiwa kulingana na sheria za kimataifa. Naamini kwamba hakuna nchi yoyote au jamii yoyote inayoweza kukubali ghasia hizi zinazokiuka sheria. Ndivyo ilivyo nchini Marekani, na ndivyo inavyopaswa kuwa kwa Hong Kong''.

Madhara kwa biashara

Maandamano haya yamezifanya biashara na masoko ya fedha kufunga milango, na wanauchumi wanaonya kuwa ikiwa maendamano hayo yataendelea, yanaweza kuyatia wasiwasi makampuni ya kimataifa, yakihofia kuwa hali hiyo ya vurugu itatokea mara kwa mara.

Tayari China imesimamisha misafara ya watalii wanaotoka bara kuingia Hong Kong, hatua ambayo ni pigo kubwa kwa sekta ya utalii ya kisiwa hicho ambayo imekuwa ikikuwa haraka.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/dpae

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW