Waandamanaji kadhaa wauwawa Kenya
25 Juni 2024Sehemu ya maeneo ya bunge nchini Kenya yamechomwa moto wakati maelfu ya waandamanaji wanaopinga mswada tete wa fedha, walipovamia katika maeneo hayo.
Wabunge waliokuwa ndani ya bunge, inasemekana walitoroshwa na kupelekwa sehemu salama. Hatua hiyo ya waandamanaji kuvamia maeneo ya bunge ni shambulizi la moja kwa moja kwa serikali ambalo halijawahi kuonekana kwa miongo kadhaa.
Polisi wa Kenya wafyatua mabomu ya machozi kwa waandamanaji
Moja ya matakwa ya waandamanaji ni wabunge hao kutoupigia kura mswada huo wa fedha, unaotaka kuwatoza wananchi ushuru zaidi katika nchi hiyo ambayo tayari watu wake wanapambana na kupanda kwa gharama ya maisha.
Waandamanaji wakasirishwa na hatua ya wabunge kupitisha mswada wanaoupinga
Waandamanaji waliwashinda nguvu polisi na kuingia bungeni muda mfupi baada ya wabunge kupitisha muswada huo, ambao sasa unasubiri saini ya Rais William Ruto kuwa sheria kamili. Waandamanaji hao hata hivyo waliwaruhusu wabunge wa upinzani walioupinga mswada huo kuondoka katika maeneo hayo waliyoyazingira.
Kijana wa pili athibitishwa kufa katika maandamano ya Kenya
Ofisi ya gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye pia ni mwanachama wa chama tawala, imechomwa. Ofisi hiyo ipo karibu na maeneo ya bunge. Polisi kwa sasa wanatumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuendelea kuwatawanya waandamanaji waliojawa na hasira, waliosikika wakisema watawaandama wanasiasa wote.
Tume ya haki za binadamu ya Kenya KHRC, imesema katika taarifa iliyoitoa kupitia ukurasa wa X kuwa "polisi wamewapiga risasi waandamanaji wanne na kumuua mmoja, tunalaani vikali mauaji ya polisi".
afp/ap