1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji kiasi 37 wauwawa Sudan

25 Desemba 2018

Vikosi vya usalama vyakabiliana na waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu Khartoum wakielekea ikulu kushinikiza rais Bashir ajiuzulu madarakani. Wasudan walalamika kuuchoka utawala wa rais aliyeitawala nchi miaka 29

Sudan Khartum Anhänger  Sadiq al-Mahdi  Opposition
Picha: Reuters/M. Nureldin Abdallah

Vikosi vvya usalama vya Sudan vimewauwa watu kiasi 37 waliokuwa wakishiriki kwenye maandamano ya kupinga sera za kiuchumi za serikali. Watu hao waliuwawa kwa kupigwa risasi kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International. Katika kipindi cha wiki moja iliyopita Wasudan wamekuwa wakiandamana katika mitaa mbali mbali ya nchi hiyo baada ya kupanda bei vitu mbali mbali ikiwemo mkate uliopandishwa bei mara tatu zaidi ya iliyokuwepo awali. Serikali ya Sudan ilitangaza hali ya hatari jumatano iliyopita katika mikoa miwili kufuatia maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea kote nchini humo.

Naibu mkurugenzi wa shirika la Amnesty International Sarah Jackson amesema kutokana na watu chungunzima kuuwawa serikali inapaswa kukoma kutumia nguvu dhidi ya maandamano na kuzuia kusababisha umwagikaji wa damu usiokuwa wa lazima. Shirika hilo limesema serikali ya mjini Khartoum badala ya kuwazuia watu kuandamana inapaswa kulenga kumaliza ukandamizaji wa haki za binadamu  na kuutatua mgogoro wa kiuchumi ambao ndio chachu kubwa ya maandamano hayo.

Gharama ya mkate yapanda mara dufuPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Leo Jumanne yalizuka makabiliano katika mji mkuu Khartoum kati ya polisi na maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuandamana kuelekea kwenye ikulu kumshinikiza rais Omar al Bashir ajiuzulu madarakani kwa mujibu wa wanaharakati na vipande vya vidio vilivyorushwa kwenye mitandao. Vidio hizo zimeonesha makundi ya mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika pembezoni mwa barabara na wakielekea upande wa ikulu ya rais iliyoko katikati ya mji wa Khartoum.

Waandamanaji hao walionekana wakiimba nyimbo za kizalendo huku wakipaaza sauti wakisema wanaandamana kwa amani dhidi ya waporaji na kwamba wananchi wanataka kuuangusha utawala. Kauli mbiu hiyo iliyosikika ni sawa na ile iliyokuwa maarufu mwaka 2010 na 2011 wakati wa maandamano ya vuguvugu la harakati za kudai demokrasia katika nchi za kiarabu. Idadi kubwa ya vikosi vya usalama imepelekwa katika mji mzima wa Khartoum kukabiliana na maandamano hayo ambapo wanajeshi wameonekana wakiwa kwenye magari maalum ya kasi ndogo.

Picha: Reuters/Stringer

Polisi wametumia gesi ya kutowa machozi kuwatawanya baadhi ya waandamanaji. Ikumbukwe maandamano haya yaliitishwa na muungano wa vyama vya wasomi huru  na kuungwa mkono na vyama vikubwa vya  kisiasa vya upinzani  nchini Sudan ,Umma na Democratic Nationalist. Waandaaji wa maandamano hayo wanataka kuwasilisha ombi la kumtaka Bashir aliyekaa madarakani kwa miaka 29 aachie ngazi.

Maandamano ya leo Jumanne (25.12.2018) yanafuatia takriban wiki moja ya maandano ambayo awali yalichochewa na hali ya kupanda kwa gharama ya maisha pamoja na ukosefu wa chakula na mafuta lakini ambayo baadae yalienea na kugeuka kuwa mwito wa kumtaka rais Bashir aondoke madarakani. Siku ya Jumatatu Marekani ilitoa taarifa ya pamoja na Uingereza, Norway na Canada iliyosema nchi hizo zina wasiwasi kuhusu vikosi vya usalama vya Sudan kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AP/DPA

Mhariri:Zainab Aziz

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW