1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji Uganda wasema wataandamana licha ya zuio

22 Julai 2024

Waandamanaji nchini Uganda wamesema wataendelea na mipango yao ya kufanya mkusanyiko mnamo Jumanne ijayo ambao umepigwa marufuku na serikali.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: Darko Vojinovic/AP Photo/picture alliance

Tangazo hilo wamelitoa licha ya onyo kutoka kwa rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni aliyewaambia "wanacheza na moto", kwa mipango yao ya kufanya maandamano makubwa.

"Kuna baadhi ya makundi yamekuwa yanapanga maandamano batili, vurugu," alisema Rais Museveni kupitia hotuba kwa njia ya televisheni aliyoitoa siku ya Jumamosi.

Museveni ambaye anaitawala Uganda kwa mkono wa chuma tangu alipoingia madarakani mwaka 1986 amesema kuna ishara za waandamanaji kuwa na malengo ya kile amekitaja "kutimiza maslahi ya kigeni", bila hata hivyo kufafanua zaidi.

Mapema siku ya Jumamosi, polisi ya Uganda iliwaarifu wale wanaopanga maandamano hayo kwama haitayaruhusu. Ilisema imepata taarifa za kiintelejinsia kwamba kuna ishara ya makundi yanayotaka kutumia maandamano hayo yalipangwa kwenye mji mkuu Kampala "kuzusha machafuko nchini humo".

"Maandamano yanapaswa kuandaliwa chini ya ruhusa yetu kwa msingi kwamba hakuna vurugu itakayotokea au kuvuruga maisja ya raia wengine," amesema mkuu wa operesheni za polisi ya Uganda Frank Mwesigwa alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Waandamanaji wasema mikusanyiko ni "haki ya kikatiba"

Waandamanaji wanalituhumu Bunge la Uganda kufumbia macho rushwa na ufisadi.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Hata hivyo wale walioyapanga wameapa kuendelea nayo licha ya zuio hilo la polisi. "Hatuhitaji kibali cha polisi kufanya maandamano ya amani," amesema mmoja ya viongozi wa maandamano hayo, Louez Aloikin. "Ni haki yetu ya kikatiba".

Waandamanaji wanatuwia mkusanyiko wao utayafikia majengo ya Bunge la Taifa wanalolituhu kwa kufumbia macho vitendo vya rushwa nchini humo.

"Hatua yetu ya kwanza ya kupinga rushwa ni bunge ... na maandamano haya ni tofauti kabisa na kile kilichoelezwa na polisi," amesema Shamim Nambasa mmoja wa waandamanaji.

Shirika la kimataifa linalochungunza viwango vya rushwa na uwazi serikali la Transparency International linaiorodhesha Uganda kuwa miongoni mwa mataifa yenye viwango vya juu kabisa vya rushwa.

Katika faharasa yake ya hivi karibuni Uganda imetajwa kuwa nchini ya 141 kati ya mataifa 180 yaliyochunguzwa kwa viwango vya rushwa.

Waandamanaji wanafuata nyayo za taifa jirani la Kenya?

Waandamanaji wanaopinga rushwa nchini Uganda wamekuwa wakifuatilia kile kinachotokea kwenye nchi jirani ya Kenya ambapo maandamano ya umma ambayo wakati fulani yalikumbwa na ghasia yameitikisa nchini hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Kwa zaidi ya mwezi mmoja Kenya inaandamwa na wimbi la maandamano ya vijana.Picha: Daniel Irungu/EPA

Maandamano nchini Kenya, yaliyoanza kama mikusanyiko ya amani dhidi ya mipango tata ya serikali ya kupandisha viwango vya kodi, yamegeuka na kuwa vuguvugu kubwa la kuipinga serikali.

Waandamanaji sasa wanadai maeguzi mapana zaidi wakiitaka serikali kuchukua hatua kupambana na rushwa na dhidi ya ukatili wa polisi.

Watu wasiopungua 50 wameuawa na zaidi ya wengine 413 wamejeruhiwa tangu maandamano hayo yalipozuka kwa mara ya kwanza Juni 18 mwaka huu.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya ambayo ni taasisi ya serikali.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW