1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wakusanyika tena Sri Lanka

20 Aprili 2022

Maelfu ya watu katika maeneo tofauti ya Sri Lanka wameingia mitaani leo, ikiwa ni siku moja baada ya kuuwawa kwa mtu mmoja na wengine 13 kujeruhiwa na polisi.

Pakistan Sri Lanka Lynchjustiz
Picha: K.M. Chaudary/AP/picture alliance

Hayo yanatokea katika kipindi hiki ambacho taifa hilo la kisiwa katika Bahari ya Hindi linagubikwa na hali mbaya zaidi ya kiuchumi kwa miongo kadhaa. 

Katika maeneo mengi ya miji ya taifa hilo, waandamaji wametumia magari kuzizuia barabara muhimu kupinga kitendo vya ufyatuaji risasi kadhalika kupanda kwa bei ya mafuta na serikali kushindwa kudhibiti hali ya kuzorota kwa uchumi. Mauwaji ya sasa ya raia huyo mmoja yanatajwa kuwa ya kwanza kufanywa na polisi katika maandamano hayo ambayo yamedumu kwa majuma kadhaa.

Tukio hilo lilitokea Jumanne, katika mji wa Rambukkana, uliopo umbali wa kilometa 90, kaskazini mashari mwa mji mkuu Colombo. Katika mkasa huo kadhalika, polisi 15 walipelekwa hospitali baada ya kupata majeraha madogomadogo yaliyotokana na makabiliano na waandamanaji. Polisi imeweka marufuku ya kutotoka nje katika mji huo uliotokea mauwaji.

Kwa mkasa huo, jeshi hilo la polisi limesema waandamanaji waliizuia reli ya treni ya mizigo na barabara, na hivyo kupuuza maonyo ya kuwatawanya na badala yake waandamanaji waliwarushia mawe.

Maelfu waandamana tena.

Waandamanaji waweka vizuizi barabaraniPicha: AFP

Leo hii, maelfu ya wafanyakazi katika sekta ya kibenki, bandari, afya na waajiriwa wengine wa umma wamekusanyika katika eneo la mbele la kituo kikuu cha treni cha Colombo, na kulaani kitendo cha mauwaji cha polisi na kushinikiza Rais wa Sri Lanka, Gotabaya Rajapaksa, ajiuzulu.

Kwa kiwango kikubwa katika mfululizo wa maandamano haya ya sasa, chuki ilionekana kuelekezwa kwa kiongozi huyo wa nchi na kaka yake mkubwa, Mahinda Rajapaksa, ambaye anaongoza ukoo wenye ushawishi mkubwa nchini humo na umekuwepo madarakani kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Kataka ukoo huo, watu wengine watano ni wabunge, ambapo watatu miongoni mwao walijiuzulu katika nafasi ya uwaziri majuma mawili yaliyopita.

Sri Lanka inatajwa kuwa ipo ukingoni mwa kufilisika, ikiwa na karibu dola bilioni 7 katika jumla ya dola bilioni 25 katika deni lake la nje ambalo linapaswa kulipwa. Hali mbaya kabisa ya uhaba wa fedha za kigeni inatafsiri kuwa taifa hilo linakosa fedha za kununua bidhaa za nje ya taifa hilo.

Chanzo: AP

Mhariri: Mohammed Khelef