1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji walizingira bunge Ukraine

Admin.WagnerD3 Desemba 2013

Maelfu ya waandamanaji nchini Ukraine wamekusanyika nje ya jengo la bunge la nchi hiyo mjini Kiev siku ya Jumanne, wakati wabunge wakijadili juu ya kura ya kutokuwa na imani na serikali ya nchi hiyo.

Waandamanaji wakizuia milango ya kuingia katika moja ya majengo ya serikali.
Waandamanaji wakizuia milango ya kuingia katika moja ya majengo ya serikali.Picha: picture-alliance/dpa

Upande wa upinzani umeitisha kura ya kutokuwa na imani na serikali ya waziri mkuu Mykola Azarov kufuatia maandamano yanayoendelea kwa siku kadhaa sasa yakipinga hatua ya serikali ya Ukraine kushindwa kusaini makubaliano hayo ya kihistoria. Maandamano ya sasa ndiyo makubwa zaidi kuwahi kulikumba taifa hilo la zamani la kisovieti tangu mapinduzi ya rangi ya machungwa yaliyoungwa mkono na mataifa ya magharibi mwaka 2004.

Mwandamanji akipiga kelele katika kuunga mkono ushirikiano kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya.Picha: Reuters

Viongozi wa upinzani, akiwemo bingwa wa zamani wa mchezo wa ngumi Vitali Klitschko waliwasilisha muswada wa azimio hilo, wakisema serikali imewasaliti raia wa Ukraine kwa kukataa kusaini makubaliano hayo na Umoja na Ulaya kwa shinikizo la Urusi. Lakini haikubainika wazi iwapo upande wa upinzani ungepata uungwaji mkono wa kutosha kuweza kupitisha muswada wa kura hiyo.

Hofu ya mapinduzi
Maandamano makubwa yaliyofanyika mwishoni mwa wiki yalisababisha makabiliano ya vurugu na polisi, ambao walitumia hewa ya kutoa machozi na magruneti yanayopoteza fahamu, ingawa hali ilitulia siku ya Jumatatu.

"Watu wameingia mitaani kwa sababu wamekatishwa tamaa kwa kuwa serikali zinabadilika mara kwa mara, na mawaziri wanabadilika, lakini hali haijabadilika - inaendelea kuwa mbaya zaidi - rushwa na ukosefu wa utawala wa sheria - Laazima tubadilishe mfumo mzima," alisema Vitali Klitschko.

Waziri mkuu Azarov alisema siku ya Jumatatu, kuwa hali iliyopo nchini Ukraine kwa sasa inaashiria mapinduzi, huku rais wa Urusi Vladmir Putin akisema kuwa maandamano hayo yanaonekana kama mauaji ya kikatili yanayolenga kuangamiza jamii ya watu kuliko mapinduzi. Kwa upande wake, ikulu ya Marekani White House ilisema haichukulii maandamano ya amani kuwa ni mapinduzi.

Polisi wakichunga mbele ya waandamanji mjini Kiev.Picha: Reuters

Maelfu ya polisi wa kupambana na ghasia wamezungushwa jengo la bunge katikati mwa mji wa Kiev, na wengine wamewekwa kuzunguka majengo mengine ya serikali.

Azimio mashakani
Upinzani unahitaji kura 226 katika bunge lenye jumla ya wabunge 450 ili kupitisha kura ya kutokuwa na imani na serikali. Lakini Nikolai Tomenko, mbunge kutoka chama cha kiongozi wa upinzani alieko kifungoni Yulia Tymoshenko, alisema upinzani unaweza tu kupata kura 215 kati ya zinazohitajika katika bunge hilo linalodhibitiwa na chama cha rais Viktor Yanukovych cha Regions.

Wakati hali ikiwa bado ni tete, rais Yanukovychi anajiandaa kuondoka nchini humo kuelekea China kwa mazungumzo na viongozi wa China juu ya uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae, afpe, rtre
Mhariri: Saum Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi