1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji waongeza shinikizo kwa rais Lukashenko

24 Agosti 2020

Makumi kwa maelfu ya waandamanaji wameminika kwenye mjini mkuu wa Belarus, Minsk, kumtaka rais Alexander Lukashenko kujiuzulu katika mfululizo wa maandamano ya umma ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yanayozoniwa.

Belarus Minsk | Proteste gegen Präsident Lukaschenko
Maelfu ya waandamanaji mjini Minsk Picha: picture-alliance/dpa/D. Lovetsky

Makundi makubwa ya watu yakiwa yamebeba bendera za upande wa upinzani zenye rangi nyekundu na nyeupe yalifurika katika uwanja wa uhuru na kisha kukusanyika katikati ya mji huku wakipaza sauti na kaulimbiu za kudai uhuru.

Wiki mbili tangu kufanyika uchaguzi unaozozaniwa uliomrudisha madaraka rais Lukashenko, waandamanaji walirejea mitaani kwa idadi kubwa licha ya kitisho kutoka vyombo vya dola.

Wengi ya walioshiriki maandamano ya jana wanataka kufanyika kwa uchaguzi mwingine na kukomeshwa kwa vitendo vya vurugu nchini Belarus.

Mmoja ya waandamanaji aliyejitambulisha kwa jina moja la Olga alisema "Sauti ya umma imehujumiwa na tunataka kurejesha haki. Sote tuliokuwa hapa, ndiyo maana nami niko hapa. Tunataka uchaguzi mpya, uchaguzi halali na uchaguzi wa kuaminika nchini mwetu. Ndiyo maana niko hapa"

Lukashenko aendeleza vitisho 

Rais Alexander LukashenkoPicha: AFP/BELTA

Wakati hayo yakijiri shirika la Habari la Taifa lilimuonesha rais Lukashenko akiwa ameshika bunduki ya rashasha na kikoti cha kuzuia risasi muda mfupi baada ya kuteremka kutoka kwenye helikopta iliyompeleka kushuhudia maandamano katikati ya mji.

"Walikimbia kama panya " alisikika akisema rais Lukashenko akizungumzia kutawanyika kwa hiyari kwa waandamanaji majira ya jioni baada ya mvua kubwa kuanza kunyesha mjini Minsk.

Hapo kabla Lukashenko alituma kikosi chake cha kutuliza ghasia kutawanya waandamanaji wanaopinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi wa asilimia 80, ambayo hata hivyo upinzani unasema yalikubikwa na wizi wa kura.

Maafisa wa Belarus waliwaonya raia wa nchi hiyo dhidi ya kushiriki kile walichokitaja kuwa ´maandamano yasiyo halali´ na wizara ya ulinzi ilitahadharisha kuwa itaingilia kati na kuwakabili waandamanaji.

Kiongozi huyo pia aliamuru jeshi kujiweka tayari kudhibiti maandamano ya umma ambayo yamegeuka changamoto kubwa kwa utawala wake wa miaka 26 kwenye taifa hilo la uliokuwa muungano wa kisovieti.

Kiongozi wa upinzani asema raia wameacha kuogopa 

Kiongozi wa upinzani aliyechuana na rais Lukashenko katika uchaguzi wa Agosti 9, Svetlana Tikhanovskaya alizungumza kutoka nchini Lithuania aliko uhamishoni na kusema vitisho vilivyotolewa na serikali vimezoeleka lakini raia wa taifa hilo wameacha kuogopa.

Waandamanaji nchini Lithuania Picha: Getty Images/AFP/P. Malukas

Matamshi ya Tikhanovskaya yalitolewa wakati maelfu ya raia wa mataifa ya Baltiki pia walifanya maandamano makubwa kuonesha mshikamano na Belarus.

Nchini Lithuania, wahudhuriaji walishikana mikono na kutengeneza mstari wenye urefu wa kilometa 30 kutoka mji mkuu Vilnius hadi kwenye mpaka na Belarus.

Mikusanyiko ya kuonesha mshikamano imefanyika pia kwenye mataifa mengine ya Ulaya ikiakisi maandamano ya mwezi Agosti mwaka 1989 ambapo zaidi ya raia milioni moja wa mataifa ya Baltiki ya Lithuania, Latvia na Estonia waliunganisha mikono kupinga utawala wa iliyokuwa dola ya kisovieti.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW