1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji warejea mitaani Lebanon kwa kutumia magari

21 Aprili 2020

Mamia ya Walebanon wameingia mitaani kuandamana wakiwa ndani ya magari yao ili kuepusha misongamano na kukaribiana kutokana na janga la Corona.

BdTD Libanon Proteste
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Hussein

Misururu ya magari ya waandamanaji hao imeutawala mji mkuu Beirut,wakipiga honi za magari na kupeperusha bendera  katika uwanja wa mashujaa ambako ni kitovu cha vuguvugu la maandamano yaliyoanzishwa takriban kipindi cha nusu mwaka kilichopita. 

Mtu mmoja miongoni mwa waandamanaji Hassan Hussein Ali mwenye umri wa miaka 22 alinukuliwa akisema, anafurahi kurudi tena kwenye uwanja wa maandamano. Kijana huyo anashiriki maandamano akiwa amebeba kipaza sauti huku amevaa barakoa.

Amesikika kusema kupitia kipaza sauti kwamba Corona imeuwa kila kitu lakini imeshindwa kuwazuia wanasiasa wao mafisadi, na kwa hivyo haiwezi kuwazuia hata wao waandamanaji.''

Waandamanaji chungunzima walioko ndani ya magari yao walisikika wakipiga kelele, wakiwa wamevaa vibarakoa vya kila aina ya rangi na baadhi ya wengine wakiwa wamevalia mpaka glavu za kujikinga mikono walizunguka kwa magari kote mjini Beirut na kwenye eneo la pwani ya mji huo.

Picha: Getty Images/AFP/I. Amro

Waandamanaji hao walisimama karibu na eneo ambako wabunge walikuwa wakiendesha kikao cha kujadili masuala tete yaliyopo nchini humo ikiwemo suala la kutoa msamaha, kuhalalisha matumizi ya bangi na kuondolewa kwa kinga ya kushtakiwa mawaziri na wabunge wanaotuhumiwa kuhusika na rushwa na ufisadi.

Nguvu kubwa isiyotikisika

Itakumbukwa kwamba maandamano makubwa ya nchi nzima yalizuka Lebanon   Oktoba 17 mwaka jana kupinga  mtindo wa kundi la watu fulani kuzishikilia siasa za nchi hiyo  lakini yakashindwa kuleta  mageuzi makubwa nchini humo.

Kuishiwa nguvu kwa maandamano hayo pamoja na mgogoro wa kiuchumi ulioitumbukiza nchi hiyo katika hali mbaya tayari ni mambo yaliyolifanya vuguvugu la maandamano hayo kujiweka kando hata kabla ya kuanzishwa kwa hatua za kuwataka watu wabakie majumbani kutokana na janga la virusi vya Corona.

Lakini wafuatiliaji wa hali ya mambo katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati wanasema hatua zilizochukuliwa na mabenki za kudhibiti uwezo wa wananchi  kupata pesa za kigeni pamoja na kushuka kwa thamani ya sarafu kunaweza kukachochea wimbi jingine kubwa la maandamano ikiwa zuio la watu kutoka nje litaondolewa.

Maandamano ya Jumanne (21.04.2020) yameonesha kuikumbusha serikali mpya inayokabiliwa na mkwamo kwamba waandamanaji bado ni nguvu kubwa isiyotikisika.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga