1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji warudi majiani Tanzania

Jacob Safari Reuters
30 Oktoba 2025

Polisi katika mji mkuu wa kibiashara Tanzania, Dar es Salaam, mapema Alhamis walifyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji, siku moja baada ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na maandamano.

Moto uliowashwa na waandamanaji barabarani
Moto uliowashwa na waandamanaji barabaraniPicha: AP

Dazeni kadhaa za waandamanaji walirudi kuandamana katika barabara za mitaa ya Mbagala, Gongo la Mboto na Kiluvya ila polisi waliwafyatulia risasi na mabomu ya kutoa machozi. Haya ni kulingana na chanzo cha shirika la habari la Reuters.

Ubalozi wa Marekani umesema barabara kuu ikiwemo ile inayoelekea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere huko Dar es Salaam, zimefungwa.

Ripoti zinaarifu kuwa baadhi ya waandamanaji wamekuwa wakijadili mbinu za maandamano zaidi ikiwemo kuelekea katika majengo ya serikali, kupitia app inayoitwa Zello, ambayo inaikubalia simu ya kisasa ifanye kazi kama redio ya mkononi ya kupokea na kuleta habari.

Wafanyakazi wafanye kazi majumbani

Wasemaji wa serikali ya Tanzania hawakujibu maombi ya shirika la habari la Reuters ya kutoa tamko kuhusiana na hali hiyo inayoendelea nchini humo.

Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram usiku wa Jumatano, msemaji wa serikali Gerson Msigwa aliwataka wafanyakazi wa serikali kufanya kazi kutoka nyumbani siku ya Alhamis, isipokuwa tu wale ambao majukumu yao yanwalazimu kuwa katika maeneo yao ya kazi.

Rais aliye madarakani Tanzania, Samia Suluhu HassanPicha: State House

Kituo cha televisheni cha taifa pia kilitangaza kuwa wanafunzi aidha walitakiwa kufanya masomo yao wakiwa nyumbani.

Kulizuka maandamano nchini humo katika mji wa Dar es Salaam na miji mingine wakati wa uchaguzi, huku waandamanaji wakionesha kughadhabishwa na hatua ya kuachwa nje ya uchaguzi huo kwa wapinzani wawili wakuu wa Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na kile wanachokiita ongezeko la ukandamizaji kwa wakosoaji wa serikali.

Polisi ilitoa amri ya kutotoka nje mjini Dar es Salaam, mji wa wakaazi milioni 7, kufuatua maandamano hayo yaliyokumbwa na vurugu na huduma za intaneti bado zimekatwa kote nchini humo.

Machafuko hayo ambayo yalishuhudia kuchomwa moto kwa angalau ofisi moja ya serikali ni mtihani mkubwa kwa Rais Suluhu.

Alisifiwa mno baada ya kuchukua madaraka mwaka 2021 kwa kupunguza ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa na kuwanyamazisha, mambo yaliyokuwa yamezidi chini ya mtangulizi wake John Magufuli.

Ila katika miaka ya hivi karibuni, watetezi wa haki na wagombea wa upinzani wameituhumu serikali kwa matukio ya utekwaji nyara wa watu. Mwaka uliopita Rais Samia alisema ameamrisha kufanyika kwa uchunguzi wa matukio hayo ya utekaji ila hakuna matokeo rasmi yaliyotolewa kwa umma kufikia sasa.

Marufuku chama kikuu cha upinzani

Chama kikuu cha upinzani CHADEMA kilikuwa kimetoa wito wa kufanyika maandamano siku ya uchaguzi ambao kilisema ulikuwa ni tukio tu la "kumtawaza" rais huyo.

Kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu akiwa kizimbaniPicha: Ericky Boniphace/DW

CHADEMA ilipigwa marufuku ya kushiriki uchaguzi huo mwezi Aprili na marufuku hayo yalijumuisha kura ya wabunge na maafisa wake kutoka kisiwa cha Zanzibar, baada ya kukataa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, na kiongozi wake Tundu Lissu akafunguliwa mashtaka ya uhaini. Tume ya uchaguzi pia ilimpiga marufuku mgombea urais wa chama chengine cha upinzani ACT Wazalendo, na kukasalia vyama vidogo vidogo tu kupambana na Rais Samia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW