1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wataka kuachiwa Deniz Yucel Uturuki

Mohammed Abdulrahman
1 Machi 2017

Maandamano yamefanyika karibu kote nchini Ujerumani na miji mingine mikubwa nchini Austria na Uswisi, kumuunga mkono mwandishi habari Mjerumani mwenye asili ya Uturuki Deniz Yucel alieko gerezani Uturuki.

Deutschland | Demo für die Freilassung von Welt-Korrespondent Deniz Yücel
Picha: Reuters/F. Bensch

Mjini Berlin  karibu  magari 100 na baiskeli 19 zilishiriki katika maandamano hayo kote katika mji huo mkuu wa Ujerumani, kama sehemu ya  kile kinachojulikana kama " Juhudi za  kupigania kuachiwa huru Deniz". Baadae waandamanaji wakakusanyika kwenye Ubalozi wa  Uturuki kudai  Yucel aachiwe huru .

Baadhi ya mabango yalikuwa na maandishi " Uhuru kwa  waandishi wote waliokamatwa Uturuki".

Miongoni mwa waliohutubia ni  pamoja na  Kiongozi wa Chama cha Kijani  cha Ujerumani Cem Ozdemir ambaye alitoa wito wa kuachiwa waandishi habari na  wanaharakati wanaopigania demokrasia ambao kwa wakati huu wako gerezani.

Mwandishi wa gazeti la Die Welt Deniz Yucel mwenye uraia wa Uturuki na Ujerumani yuko rumande nchini Uturuki wakati uchunguzi wa kesi yake unaendelea.Picha: picture-alliance/dpa/C.Merey

Maandamano yalifanyika pia katika  miji ya  Cologne, Frankfurt na Munich.

Awali waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel alimwita balozi wa Uturuki kwenye Wizara ya kigeni mjini Berlin na kuzungumzia  kisa cha Yucel. Baada ya mazungumzo yao Gabriel alisema, kuwekwa ndani Yucel nchini Uturuki ambapo anaweza kubakia hadi miaka mitano kabla ya kuachiwa huru au kufikishwa mahakamani, kumesababisha mvutano mkubwa katika uhusiano wa nchi hizo mbili na kwamba na moja wapo ya mitihani mikubwa ya wakati huu.
 

"Uamuzi huu sio tu wakushangaza  pia si wa lazima na usio na kipimo. Mtu anayefanyakazi yake ya uandishi habari sio tu Ujerumani bali pia Uturuki, ana haki za kinga na uhuru wakutoa maoni, " alisema waziri Gabriel.

Amri "chungu na ya kuvunja moyo"

Yucel ambaye ni mwandishi habari mwakilishi wa  gazeti la Ujerumani Die welt na  mwenye uraia pacha-  wa Ujerumani na Uturuki alikamatwa Februari 14 na kuwekwa  rasmi kizuizini  siku 13 baadae, hatua iliokosolewa vikali  nchini Ujerumani. Kansela Angela Merkel aliitaja  amri hiyo ya mahakama  kuwa "chungu na yenye kuvunja moyo".

Rais Joachim Gauck  kwa upande wake alitamka",   Sisi nchini Ujerumani tunashindwa kufahamu kwanini kuna haja ya kuvishambulia vyombo vya habari". akaongeza kwamba kile kinachotokea Uturuki hivi sasa kinazusha  shakashaka iwapo kweli Uturuki inataka kubakia kwenye utawala wa kisheria.

Waandamanaji wakishinikiza kuachiwa kwa Yucel na waandishi wengine wanaoshikiwa nchini Uturuki.Picha: picture-alliance/dpa/A. Arnold

Mwandishi huyo wa habari aliandika ripoti mwezi Septemba kuhusu kuandamwa na vitisho vya  mitandaoni  dhidi ya wanaoikosoa serikali, kukitumiwa anuwani za baruapepe za Waziri wa nishati Berat Albayrak ambaye ni  mkwewe Rais Recep Tayip Erdogan.

Baruapepe tatu zilichapishwa na  mtandao wa ufichuzi wa Wikileaks na kundi moja la  upekuzi wa mitandao  nchini Uturuki. Yucel anatuhumiwa kwa kueneza propaganda za Chama cha wafanyakazi cha Wakurdi -PKK- kilichopigwa marufuku na  kile cha  kiongozi wa kidini  Fethullah Gulen ambaye serikali ya Uturuki inamtuhumu kuwa nyuma ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa  Julai  mwaka jana 2016.

Makundi yote mawili yanatajwa na serikali ya Uturuki kuwa ya kigaidi. Leo  Umoja wa Ulaya umeitaka Uturuki kufuata  utawala wa kisheria. Kamishna anayehusika na  kutanuliwa kwa Umoja huo Johannes Hahn aliliambia gazeti la Welt  kwamba,  Umoja wa Ulaya unashtushwa na  idadi kubwa ya waandishi habari waliokamata na kuwekwa ndani nchini Uturuki.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp,dpa

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW