1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 2 wauawa katika Ghasia Burundi

Admin.WagnerD22 Mei 2015

Ghasia zimeshuhudiwa tena Alhamis katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, baina ya waandamanaji wanaopinga hatua ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kugombea mhula wa tatu madarakani. Waandamanaji wawili wameuawa.

Polisi nchini Burundi imeendelea kufukuzana na rawaandamanaji mitaani
Polisi nchini Burundi imeendelea kufukuzana na rawaandamanaji mitaaniPicha: picture-alliance/D. Kurokawa

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la msalaba mwekundu, watu wawili waliuawa leo katika makabiliano baina ya vijana waliokuwa wakirusha mawe, na askari jeshi na polisi ambao walikuwa wakiripua mabomu ya kutoa machozi, na kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji hao. Wananchi walioshuhudia mauaji hayo, wamelalamika wakitaka hali hiyo ikomeshwe.

''Jamani haya ni mambo ngani? Kuingia katika nyumba ya familia yenye watoto, na kumuuwa raia, na kuangamiza maisha yake. Hapana, haiwezakani, lazima hali hii isimamishwe tupate amani katika nchi yetu. Burundi yetu imechoka, tunataka amani'' Amesema msichana ambaye hakutaka jina lake litajwe. Mvulana ambaye pia hakupenda kutangaza jina lake ameongeza, ''Huyu hapa mtu wamemuuwa, mbele ya macho yetu kabisa. Obama tafadhali saidia, jumuiya ya kimataifa saidia, saidieni kutuondolea huyu mwanaume''.

Shirika la Msalaba mwekundu latoa lashuhudia vifo

Msemaji wa Shirika la Msalaba mwekundu la Burundi Alexis Manirakiza, amesema shirika hilo limeshuhudia watu 20 wakiuawa, mnamo kipindi cha takribani mwezi mzima cha machafuko na maandamano yanayolenga kumzuwia rais Pierre Nkurunziza kugombea mhula wa tatu, ambao wapinzani wanasema unakiuka katiba ya nchi hiyo.

Shirika la Msalaba mwekundu limeshuhudia watu 20 wakiuawa mjini BujumburaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Mfanyakazi mwingine wa shirika la msaada amesema idadi ya waliouawa katika mzozo huo unaotishia kuitumbukiza Burundi katika mgogoro mwingine wa kikabila, inaweza kuwa wau 40.

Rais Nkurunziza asakata kabumbu

Hata hivyo rais Nkurunziza haonekani kusumbuliwa na mzozo huu, kwani jana alicheza mechi ya soka na marafiki zake, kabla ya kutoa hotuba kwa taifa.

Katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa raia wa Burundi kuungana, akisema maafa yaliyotokea katika historia chungu ya nchi hiyo, vikiwemo vita vilivyomalizika mwaka 2005 baada ya kuangamiza maisha ya watu 300,000; kamwe hayawezi kufumbiwa macho.

Licha ya mzozo huo, rais Pierre Nkurunziza ameonekana uwanjani akisakata kabumbuPicha: Reuters/G. Tomasevic

Wapinzani wake wametupilia mbali rai yake katika hotuba hiyo. Mmoja wao, Jean Claude Gakiza ameliambia shirika la habari la Reuters, kwamba mtu anayekiuka katika ya nchi, hawezi kuwatakia mema raia. ''Tunachotaka ni kumuona akiachana na azma yake ya kugombea mhula wa tatu'', amesema Gakiza.

Wakati huo huo waziri mpya wa ulinzi wa Burundi, Emmanuel Ntahomvukiye ambaye ni raia wa kwanza kuteuliwa kuiongoza wizara hiyo nchini Burundi, amewataka wanajeshi wote wa nchi hiyo kuungana, akisema usalama wa Burundi unategemea umoja wao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi