1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGeorgia

Waandamanaji wavamia bunge mkoa wa Abkhazia

15 Novemba 2024

Waandamanaji katika eneo lililojitenga na Georgia la Abkhazia wamevamia jengo la bunge huku wanasiasa wa upinzani wakimtaka rais kujiuzulu kufuatia makubaliano ya uwekezaji na taifa la Urusi ambayo yalipingwa na umma.

Maandamano ya Abkhazia
Waandamanaji waliovamia majengo ya bunge kwenye mkoa uliojitenga na Georgia wa Abkhazia.Picha: Anzhela Kuchuberia/TASS/IMAGO

Waandamanaji walitumia lori kuvunja uzio wa chuma unaolizunguuka jengo la bunge katika mji mkuu wa Sukhumi. Picha za video zimewaonyesha watu wakipanda kupitia madirisha huku wakiimba.

Eshsou Kakalia, kiongozi wa upinzani na naibu wa zamani wa mwendesha mashtaka mkuu, amesema jengo la bunge huko Abkhazia lipo chini ya udhibiti wa waandamanaji. Ofisi ya rais imesema katika taarifa kwamba wanajiandaa kuyafutilia mbali makubaliano hayo.

Urusi iliitambua Abkhazia na eneo lingine lililojitenga la Ossetia Kusini, kama majimbo huru mnamo mwaka 2008 baada ya vikosi vya Moscow kuzuia jaribio la Georgia la kutaka kuchukua tena udhibiti wa Ossetia Kusini katika vita vilivyodumu kwa siku tano.