Waandamanaji zaidi wauawa nchini Myanmar
27 Machi 2021Kwa mujibu wa taarifa, zaidi ya watu 70 wameuawa baada vikosi vya usalama kuwafyatulia risasi waandamanaji katika sehemu mbalimbali za nchini Myanmar. Wakati huo huo katika kuadhimisha siku ya majeshi, leo Jumamosi tarehe 27.03.2021, kiongozi wa jeshi la nchi hiyo,Jenerali Min Aung Hlaing, aliyetwaa mamlaka ameahidi kuitisha uchaguzi mpya lakini amewaalani waandamanaji. Amesema jeshi linataka kushikamana na taifa lote kwa ajili ya kuilinda demokrasia.
Soma zaidi: Wanaharakati watoa wito wa maandamano zaidi Myanmar
Jamii ya kimataifa imelaani mauaji hayo huku balozi za Jumuiya ya Ulaya pamoja na Uingereza zikielezea kusikitishwa na mauaji ya raia wakiwemo watoto ambayo yamefanyika sanjari na maadhimisho ya 76 ya Siku ya vikosi vya jeshi nchini Myanmar. Naibu waziri wa ulinzi wa Urusi Alexander Fomin pia alihudhuria gwaride la maadhimisho na amekutana na viongozi wa jeshi la Myanmar na kuwaonga mkono.
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya uliopo nchini Myanmar umesema siku hii itabaki kwenye kumbukumbu za watu kama ni siku ya vitendo visivyoweza kusahaulika vya ugaidi na fedheha kwa raia wa Myanmar. Mabalozi wa Umoja wa Ulaya na Uingereza nchini Myanmar wamesema jeshi limezidi kujivunjia hadhi yake kwa kuwapiga risasi raia ambao hawakujihami.
Ukatili dhidi ya wapinzani unaendelea nchini humo hata baada ya watawala wa kijeshi kusema watawalinda watu na kuahidi kuitetea demokrasia. Katika jiji la Mandalay ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini humo watu 10 waliuliwa na majeshi ya usalama. Wengine waliuliwa kwenye miji ya Sagaing na Yangon.
Soma zaidi:Vikosi vya usalama Myanmar vyaendeleza matumizi ya nguvu
Mwanaharakati mmoja kutoka mji wa Mandalay ameiambia DW kwamba wanajeshi walikuwa wanavamia vitongoji wakiwa wamevalia nguo za kiraia na silaha walizozificha. Mwanaharakati huyo amesema wanajeshi wanawalenga siyo tu waandamanaji bali sasa wanavamia vitongoji na kufyatua risasi, kuwapiga watu na kupora kila kitu. Mwanaharakati David amesema wanajeshi wanachoma moto sehemu kadhaa mitaani.
Tarehe mosi mwezi uliopita Wanajeshi nchini Myanmar walitwaa mamlaka kutoka kwa serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Na tungu wakati huo maandamano makubwa yamekuwa yanafanyika nchini kote. Aliyekuwa kiongozi wa serikali hiyo Aung San Suu Kyi pamoja na wengine wametiwa ndani.
Vyanzo:/https://p.dw.com/p/3rG7X/AP