Waandishi 13 wa Kimarekani hatarini kutimuliwa China
18 Machi 2020Kufukuzwa kwa wandishi hao ni ulipaji kisasi dhidi ya uamuzi wa utawala wa rais wa Marekani Donald Trump, kuwawekea ukomo wa vibali vya kuishi Marekani waandishi wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya China.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Geng Shuang hakusema ni waandishi wangapi wa Kimarekani watafukuzwa, lakini ilielezwa awali kuwa ni wale kutoka magazeti ya The New York Times, Wall Street Journal pamoja na The Washington Post.
Vibali vya kuishi China vya waandishi hao walioathirika vitamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu wa 2020, na China imesema vile vile kuwa hawatoruhusiwa kufanya kazi mjini Hong Kong.
Shirika la waandishi wa habari wa kimataifa nchini China, FCCC limesema waandishi wanaolengwa na uamuzi huo wa China ni 13, lakini idadi yao inaweza kuongezeka kulingana na tafsiri ya kundi linalohusika. FCCC imesema waandishi hao wa vyombo vya habari vya Marekani wametakiwa kusalimisha vibali vyao vya kufanyia kazi nchini China katika muda usiozidi siku kumi.
Hii ni mara ya kwanza kwa China kuwafukuza waandishi wa habari wengi wa kigeni kwa wakati mmoja, kwa sababu tangu mwaka 2013 hadi wakati huu ni tisa tu waliokwishatimuliwa.
Katika tangazo lake, shirika hilo la waandishi wa kimataifa nchini China limekosoa serikali za nchi mbili, Marekani na China, likisema hakuna mshindi katika vita vya kidiplomasia, vinavyowatumia waandishi wa habari kama kafara.
Mapema mwezi huu serikali ya Rais Trump ilibainisha kuwa itatoa viza zisizozidi 100 tu kwa waandishi wa habari wa vyombo vya serikali ya China, uamuzi uliomaanisha kuwa waandishi habari wapatao 60 watalazimika kufungasha vyao na kurejea China.
Kufukuziana waandishi wa habari ni uwanja mpya wa vita baina ya mataifa hayo mawili yanayoongoza kiuchumi duniani, baada ya miaka kadhaa ya mivutano katika vikwazo vya kibiashara na kiushuru.
Nchi hizo, Marekani na China, zimekuwa pia zikibadilishana maneno makali, kuhusiana na janga la virusi vya corona ambavyo mripuko wake ulianzia China na kusambaa kote duniani.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amepinga kulinganishwa kwa hatua zilizochukuliwa baina ya nchi yake na China, akitoa hoja kuwa nchini Marekani waandishi wote wa habari wanao uhuru ambao haupo kabisa China.
Vyanzo: rtre, ape