1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi habari Tanzania: "Uandishi si uhalifu"

Angela Mdungu
26 Agosti 2019

Waandishi wa habari nchini Tanzania wanasema wamekuwa wakipitia kwenye wakati mgumu kutokana na kuongezeka kwa matukio ya kukamatwa na vyombo vya dola na kisha kushikiliwa korokoroni kwa siku kadhaa.

Tanzania We need freedom of press
Picha: DW/A. Juma

Hayo yanajiri baada ya kushuhudiwa waandishi wengine wawili wakikamatwa kutokana na kazi zao hali ambayo imezidisha wasiwasi miongoni mwao hasa wakati huu ambapo taifa hilo likieleleea katika uchaguzi wa serikali za mitaaa utakaofanyika Novemba 24 na ule mkuu uliopangwa kufanyika mwakani.

Huku kukiwa na kampeni inayoendelea kuvuma kwenye mitandao ya kijamii kupinga madhila hayo yanayowakuta wanahabari, bado hali haijawa shwari kwa upande wao kutokana na kuongezeka kwa visa vya kukamatwa na kutupwa korokoroni.

Mwishoni mwa wiki ilishuhudiwa mwandishi mmoja akikamatwa na polisi wakati alipofika sehemu ambako viongozi wa chama cha ACT Wazalendo wakijiandaa kufanya shughuli zao za kichama. Mwandishi huyo ambaye ameachiwa kwa dhamana leo mchana, ameungwanishwa katika kosa moja na viongozi wa chama hicho wanaodaiwa kukusanyika bila kibali.

Wengi wamekuwa wakihoji hatua ya kutiwa mbaroni mwandishi huyo aliyefika kwenye eneo la tukio kwa ajili ya kutimiza majukumu yake ya kikazi.

Nini hatma ya waandishi habari nchini humo?

Mfululizo wa matukio ya namna hiyo ikiwamo lile lamwandishi mwingine aliyekamatwahivi karibuni jijini Dar es Salaam na kisha kusafirishwa hadi huko Iringa kwa madai ya kutoa taarifa iliyowatuhumu askari polisi, kumeibua mjadala kuhusu hatma ya waandishi wa habari na usalama wao.

Johnsis Ndodo wakili wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu anasema haya yanayoshuhudiwa sasa ni matokeo ya kile alichosema sheria kandamizi zilizopitishwa katika miaka ya hivi karibuni.

Erick Kabendera, mmoja wa waandishi wa habari wa Tanzania alipokuwa mahakamani jijini Dar es salaam 5.8.2019Picha: DW/S. Khamis

Ingawa katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la idadi ya vyombo vya habari na waandishi wenyewe, bado waandishi hao hawajihisi kama wako huru kukosoa na kuwasilisha ujumbe wa mada zinazohusika.

Kaimu mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania, Deodatus Balile amesema mwenendo huu wa kuendelea kuwaaandama wanahabari inazidisha wasiwasi hasa wakati huu wa kuelekea kwenye chaguzi za usoni ambako waandishi hao wana jukumu kubwa la kuchambua mambo.

Wakati hali ikiwa hivyo, kumekuwa na kampeni inayoendeshwa kwenye mitandao ikiwa na kauli mbiu isemayo "uandishi wa habari siyo uhalifu” kampeni ambayo imelenga kutuma ujumbe kwa mamlaka za dola kutowaandama wanahabari wanapotimiza majukumu yao.

Mwandishi: George Njogopa, Dar es salaam 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW