Waandishi Habari wa DW waondolewa Afghanistan
10 Septemba 2021Katika kile kinachoweza kutajwa kuwa hali ya kushusha pumzi, kundi la waandishi habari wa DW nchini Afghanistan lilivuka mpaka leo na kuingia Pakistan hatua inayokamilisha juhudi za wiki kadhaa za kuwaondoa ambazo zilikabiliwa na vizingiti.
Kwa jumla kundi la watu 72 linalojumuisha waandishi 9 ikiwemo mwandishi habari pekee mwanamke wa DW nchini Afghanistan pamoja na familia zao wameondoka salama nchini humo.
Kundi la waandishi hao lilikwama kwa wiki kadhaa mjini Kabul baada ya kushindwa kusafiri kupitia uwanja wa ndege wa mji huo kutokana na mparaganyiko uliojitokeza katika siku za mwisho za kuondoka vikosi vya kigeni nchini Afghanistan.
Mkuu wa DW asifu hatua ya kuondolewa waandishi habari Afghanistan
DW iliwataka waandishi wake wote wa habari nchini Afghanistan kwenda mjini Kabul wakati ilipokuwa wazi kwamba kundi la Taliban lilikaribia kuchukua udhibiti wa taifa hilo.
Hata hivyo ilikuwa vigumu kuwasafirisha haraka na kundi hilo la waandishi na familia zao lilisalia kwa siku kadhaa kwenye lango la kaskazini la uwanja wa ndege mjini Kabul sehemu ambayo kulishuhudiwa tafrani kubwa kwa wote waliokuwa wakisubiri kuingia uwanjani.
Baada ya majaribio kadhaa iliafikiwa kwamba kundi hilo litaondoka nchini humo kupitia mpaka wa Pakistan wa Torkham ulio kiasi kilometa 180 kutoka mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg ameitaja hatua ya kuondoka waandishi hao nchini Afghanistan kuwa mafanikio makubwa katika wakati hali ya uhuru wa habari nchini humo ikiwa ya shaka shaka tangu kundi la Taliban lilipochukua madaraka.
Hali ni shwari Afghanistan huku mataifa ya magharibi yakiendelea kuondoa watu
Hayo yanajiri wakati mataifa ya magharibi yanaendelea kuwaondoa raia na waafghani waliokuwa washirika wake kutoka nchini Afghanistan.
Kwengineko waziri wa mambo ya kigeni wa Uhispania Jose Manuel Albares amewasili nchini Pakistan kuomba msaada wa kufanikisha kuondolewa kwa Waafghani waliofanya kazi na vikosi vya jeshi la nchi yake.
Mwanadiplomasia huyo ameapa kuwa nchi yake itafanya kila iwezalo kuwaondoa kutoka Afghanistan wale wote waliowasaidia wanajeshi wa Uhispania na ambao wako kwenye hatari ya kulengwa na watawala wa Taliban kama njia ya kulipa kisasi.
Nchini Afghanistan kwenyewe ripoti zinasema hali bado ni shwari na wanamgambo wa Taliban wanapiga doria kwenye kila pembe ya taifa hilo ikiwemo kwenye mji mkuu Kabul.
Mmoja ya waakazi wa mji huo amesema "Kuna amani, hakuna cha kuhofia. Tangu serikali ya Taliban ilipoingia hakuna wizi, wezi wamekamatwa. Kwa rehma ya Mungu kuna amani na usalama mjini Kabul"
Hata hivyo kuna malalamiko ya kupanda kwa bei za vyakula na upungufu wa mahitaji muhimu na wengi wanasubiri kuona kile serikali mpya ya Taliban itafanya kuhusu hali hiyo.