1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi walengwa katika maandamano Kenya

Wakio Mbogho31 Machi 2023

Waandishi habari nchini Kenya wameendelea kushambuliwa wakiangazia maandamano yanayoendelea katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo, licha ya matukio hayo kukemewa na makundi mbalimbali

Kenia Ausschreitungen und Gewalt, Polizei und Proteste
Picha: Reuters/T. Mukoya

Mwezi Machi, mwaka huu umetajwa kama mwezi wa giza zaidi kwa waandishi habari tangia mafanikio ya demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya. Baraza la waandishi habari limeeleza kuwa katika maandamano ya tarehe 27 mwezi huu walirekodi matukio 20 ya waandishi habari kunyanyaswa, kujeruhiwa na kukamatwa na maafisa wa polisi

Polisi wanatuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasiPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Idadi hiyo imeongezeka hii leo na kufikia 25 wengine wao wakinusurika, lakiniwa wakiwa na majeraha mabaya. Mwanahabari Eric Isinta alipigwa na bomu la kutoa machozi kwenye uso baada ya afisa wa polisi kufanikiwa kupasua dirisha la gari alimokuwa ndani. 

Baraza la MCK linaeleza kwamba wanaoonekana kulengwa zaidi ni waandishi habari wanaopiga picha na wanaorekodi matukio kwa kutumia kamera, kwa sababu washambuliaji wana nia ya kuharibu ushahidi ulionakiliwa.

David Omwoyo, afisa mkuu wa baraza la waandishi wa habari amekemea matukio haya akiyataja kama kikwazo kwa demokrasia ya Kenya. Kwa mujibu wa Omwoyo, waandishi habari sio wapinzani katika mchakato wa kisiasa unaoendelea na hawapaswi kulengwa bila sababu.

Miezi 7 ya Ruto na hali ngumu ya maisha Kenya

03:22

This browser does not support the video element.

Amesema huu ni ukiukaji wa haki zao za kibinadamu ikizingatiwa kuwa wana jukumu la kuufahamisha umma kuhusu masuala yanayohusu taifa. Ameitaka ofisi ya mkuu wa mashtaka ya umma nchini kuamuru uchunguzi wa haraka ili kusitisha tamaduni ya dhuluma dhidi ya waandishi habari kutoadhibiwa.

Makundi ya kutetea haki za binadamu pia yamekemea visa vya waandishi habari kulengwa wakati wa maandamano haya. Munira Ali Omar, afisa kutoka shirika la Haki Yetu anaeleza.

"Tunalaani matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayotekelezwa na maafisa wa polisi wanaotaka kuwanyamazisha waandamanaji. Tunapinga mashambulizi dhidi ya waandishi habari, na utekaji wa uhuru wa waandishi habari katika maandamano haya.”

Muungano wa Mawakili nchini Kenya, LSK vilevile umekosoa mashambulizi dhidi ya waandishi habari wakiziita mbinu zilizopitwa na wakati. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, mwenyekiti wa LSK Eric Theuri, amesema ni bayana kwamba hatua ya waandishi habari kuangazia maandamano haya inawanyima fursa maafisa wa polisi kutumia nguvu zaidi dhidi ya waandamanaji ndio maana wanawatishia waaandishi habari. Aidha, wamemtaka Inspekta Mkuu wa Polisi kuwajibika.

Maandamano haya vilevile yametatiza masomo katika miji ambapo inafanyika. Maafisa wa Muungano wa Waalimu nchini Kenya, KNUT wanapendekeza suluhisho mbadala ili kuepuka kuhitilafiana na mtaala wa shule.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.