Waandishi wa habari Tanzania waminywa chini ya Magufuli
3 Mei 2017Shirika hilo lenye makao makuu yake Ufaransa limeitaja Tanzania kuwa nafasi ya 83 kati ya nchi 180 katika ripoti ya mwaka ya uhuru wa vyombo vya habari.
Taifa hilo la Afrika Mashariki lilikuwa nafasi ya chini kwa mwaka uliopita, likiwakilisha nafasi ya pili katika anguko duniani baada ya Nicaragua.
Magufuli ambaye amepewa jina la utani "Tingatinga" alichaguliwa Oktoba 2015. Kipaji chake cha kukemea maovu hadharani kilimpatia sifa ya kuwa mtu asiyependelea ujinga, mpambanaji dhidi ya rushwa, vyote hivi vilimfanya kuwa mtu maarufu miongoni.
Lakini kutokuwa na uvumilivu dhidi ya ukosoaji, maamuzi ya ghafla, na kutozingazia mchakato kunawatia wasiwasi wengine ambao wanaona dalili za kimabavu katikati mwa umaarufu wake.
Ukosoaji dhidi ya Magufuli
Magufuli "hastahimili ukosoaji dhidi yake au programu zake", inasema ripoti ya RSF iliyochapishwa mwezi uliopita. Waandishi wa habari wamekuwa na wasiwasi kwa sababu hali zao zimekuwa mbaya chini ya utawala wa Magufuli. "Uhuru wa vyombo vya habari umemimywa kwa kiwango kikubwa" anasema Jenerali Ulimwengu, mwandishi wa habari mkongwe, mtaalamu wa sheria na mwanadiplomasia wa zamani, akiongeza kwamba vyombo vya habari vinakabiliwa na changamoto nyingi kwa hivi sasa.
Ulimwengu anasema, sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya 2016 hasa "inazuia watu kutekeleza uandishi wa habari huru" kwa kuipatia serikali "nguvu ya kutosha kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari".
Mwandishi wa habari mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake katika gazeti la kila siku nchini humo la Mwananchi anasema kwamba "tulilalamika chini ya utawala uliopita lakini leo tunashindwa kupumua".
Mwandishi huyo anakwenda mbali kwa kusema hata sasa wanashindwa kutangaza uovu unaofanywa na baadhi ya washirika wa rais kwa sababu rais anahisi kwamba analengwa yeye binafsi, huku akitolea mfano wa kesi ya Maxence Melo, mwanzilishi wa tovuti ya ufichuzi ya Jamii Forums.
Melo alikamatwa mwaka jana na anakabiliwa na mashitaka kwa kukataa kutoa majina ya vyanzo vya habari zake zilizofichua uozo wa rushwa katika makampuni binafsi yanayohusishwa na serikali.
RSF ilisema mwaka jana kwamba tangu kuapishwa kwa Magufuli, vituo kadhaa vya radio vimesimamishwa na watu kadhaa angalau wamefunguliwa mashitaka kwa kutoa maoni ya ukosoaji katika mitandao ya kijamii.
Juhudi za asasi za kiraia
Mwezi Agosti 2016, mtandao wa kuwalinda waandishi wa habari CPJ ulisema serikali ya rais Magufuli "imechukua mfululizo wa hatua za kuzuia mazingira ya vyombo vya habari nchini Tanzania". Waandishi wa habari nchini Tanzania wameanza kujiuzulu na kujidhibiti wenyewe katika kile wanachokiandika kutokana na hali inavyozidi kuwa mbaya. "Kalamu yangu inaweza kuleta mabadiliko gani katika nchi ambayo wabunge wanakamatwa kwa kumkosoa rais aliye na dosari", aliuliza mwandishi wa habari katika gazeti la The Guardian nchini Tanzania ambaye pia hakutaka jina lake kutajwa. "Udhibiti wa binafsi kuhusu nini useme sasa unazidi kuenea" anaongeza mwandishi huyo.
Mwezi Machi, kundi la asasi za kiraia nchini Tanzania zikiongozwa na kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC, kilianza kampeni ya mwaka mmoja ya utoaji wa semina na mijadala ya kutia msukumo wa kuheshimu uhuru wa kujieleza pamoja na kutathmini sheria mpya ikiwemo ile ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 ambayo wanasema ina vizuizi vingi na inahitaji marekebisho.
Magufuli hata hivyo haonyeshi dalili zozote za kuregeza msimamo. Mwezi Januari, aliyakosoa magazeti mawili ya Tanzania ambayo hakuyataja, na kuyatuhumu kwamba "yanahatarisha amani ya nchi" na "uchochezi".
Aliyafananisha magazeti hayo na vyombo vya habari katika nchi jirani ya Rwanda ambavyo vilitoa wito wa kuuawa kwa Watutsi kabla ya mauaji ya kimbari mwaka 1994.
"Hii haitotokea chini ya utawala wangu," alisema Magufuli, katika maneno yalio sawa na kiongozi wa Rwanda Rais Paul Kagame, ambaye anajulikana kwa kuzuia uhuru wa kujieleza wakati akisukuma ukuaji wa uchumi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Josephat Charo