1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa habari wa Reuters waendelea kushikiliwagerezani

Isaac Gamba
11 Aprili 2018

Mahakama nchini Myanmar imetupilia mbali hoja inayotaka kufutwa kesi dhidi ya waandishi wawili wa shirika la habari la Reuters waliotiwa mbaroni wakati wakichunguza mauaji dhidi ya Waislamu wa jamiii ya Rohingya,

Myanmar - Inhaftierter Reuters-Journalist Kyaw Soe Oo
Picha: Reuters

Waandishi wa habari, Wa Lone mwenye umri wa miaka 32 na Kyaw Soe Oo mwenye umri wa miaka 27, walitiwa mbaroni Desemba wakituhumiwa kwa kukiuka sheria ya nchi hiyo inayohusiana na taarifa za siri za nchi zinazohusiana na operesheni za kiusalama katika jimbo lilo kumbwa na mgogoro la Rakhine.

Myanmar imekuwa ikishutumiwa duniani kote kwa mauaji ya kiholela pamoja na kampeni ya safishasafisha ya kikabila mnamo wakati ambapo kiasi cha Warohingya 700,000 wakikimbilia Bangladesh kutoka Myanamar kufuatia operesheni inayoendeshwa na jeshi dhidi ya waasi nchini humo.

Hata hivyo, serikali ya Myanamar inakataa tuhuma hizo na kusema ilikuwa ikijitetea dhidi ya mashambulizi kutoka kwa jeshi la wokovu la warohingya yaliyofanyika Agosti 25 mwaka jana.

Waandishi hao wa habari walikuwa wakishikiliwa gerezani mjini Yangon tangu walipokamatwa wakati shauri lao likiendelea kusikilizwa huku mashahidi 17 kati ya 25 wakiwa tayari wametoa ushahidi wao.

Mawakili wa utetezi wiki iliyopita walitoa mwito kwa mahakama kufuta kesi hiyo kwa madai ya mapungufu yaliyojitokeza katika maelezo ya mashahidi lakini hata hivyo hoja hiyo ilikataliwa na mahakama inayosikiliza shauri hilo  iliyokuwa imefurika watu wakiwemo wafuasi ndugu wa washitakiwa pamoja na vyombo vya habari.

Mmoja wa majaji wanaosikiliza shauri hilo Jaji Ye Lwin amethibitisha mahakama kukataa ombi la mawakili wa utetezi la kutaka watuhumiwa waachiwe huru kabla ya mashahidi wote kutoa ushahidi.

Walikuwa wanachunguza mauaji ya warohingya

Picha: Reuters

Waandishi hao wawili wa habari walikuwa wakichunguza mauaji ya wanaume 10 wa jamii ya Rohingya yaliyofanyika Septemba 2 katika kijiji cha Inn Din kilichoko katika jimbo la Rakhine yanayodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama pamoja na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho.

Wakati huohuo katika hatua isiyo ya kawaida nchini humo ambako jeshi limekuwa likituhumiwa kwa mauaji wanajeshi saba wamehukumiwa kwenda jela pamoja na kazi ngumu kwa kuhusika kwao na mauaji hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa majeshi  iliyotumwa katika mtandao wa jamii wa Facebook jana jumanne.

Wakati akilelekea katika gari la polisi mmoja wa waandishi hao wa Reuters Wa Lone ,  alisikika akihoji  na kusema wale walioua watu wengi wamepewa kifungo cha miaka kumi wakati wao ambao walikuwa wanajaribu kutafuta habari na kuripoti wanakabiliwa na kifungo cha miaka 14 gerezani huku pia mmoja wa mawakili  Than Zaw akihoji ni kwanini waandishi hao wawili wa Reuters bado wanashikiliwa wakati taarifa zao walizoripoti ni za kweli.

Kesi dhidi ya waandishi hao imekuwa ikiendelea licha ya wito wa kimataifa kutaka waachiwe huru.

 Wiki iliyopita, shirika la habari la Reuters lilitangaza kuwa mwanasheria mmoja maarufu wa haki za binadamu Amal  Clooney ameungana na jopo la mawakili wa upande wa utetezi katika shauri hilo huku rais wa shirika la habari la Reuters, Stephen J. Adler akisema katika taarifa yake kuwa shirika hilo la habari limesikitiswa na uamuzi wa mahakama.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW