1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyombo vya habari vyataka mazingira salama na huru Tanzania

Veronica Natalis
30 Aprili 2026

Vyombo vya habari nchini Tanzania vimeitaka serikali kuweka mazingira yasiyojaa vitisho na hofu kwa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao.

Tanzania, Dodoma 2026 | Mkutano wa Mwaka wa Makampuni ya Vyombo vya Habari ukihudhuriwa na Mkurugenzi wa JAB, Kipangula.
Mkutano wa Mwaka wa Makampuni ya Vyombo vya Habari ukihudhuriwa na Mkurugenzi wa JAB, Kipangula 2026.Picha: Tanzania Journalist Accreditation Board, JAB

Wito huo umetolewa katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambayo kwa Tanzania yamefanyika mjini Arusha. Waandishi wa habari wanasema vitisho ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoiweka taaluma hiyo katika hatari.

Kwa siku mbili mfululizo, waandishi wa habari waliokutana jijini Arusha, kaskazini mwa Tanzania, katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, wamejadili kwa kina masuala yanayohusu uhuru wa wanahabari na changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa na kuvutia washiriki wengi ni vitisho na mazingira ya hofu vinavyotajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa wanahabari kutekeleza kazi zao kwa uhuru. Katika taarifa ya maazimio ya wanahabari iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo, Bi. Asha Abdalah, waandishi wa habari wameitaka serikali kuhakikisha inalinda uhuru na usalama wa wanahabari.

Serikali ihakikisha mazingira huru, salama na ya kidemokrasia

Zaidi amesema “Serikali iendelee kuhakikisha mazingira huru, salama na ya kidemokrasia kwa vyombo vya habari na wanahabari, bila hofu, vitisho na vikwazo visivyo vya lazima.”

Waandishi wengi wa habari waliozungumza na DW wamesema mazingira yaliyopo kwa sasa hayawapi uhuru wa kutosha, hasa linapokuja suala la kuikosoa serikali, wakitaja matukio ya nyuma ya wanahabari kupotea, kuuawa au kufunguliwa kesi mbalimbali. 
Maoni ya watu yanasema “Mazingira hayo yapo, na si mimi peke yangu. Waandishi wengi tunapitia hali hiyo. Unakuwa ni mwandishi wa habari lakini una hofu. Unakuwa na habari, lakini unauliza: usalama wako ukoje? Wakati mwingine unaamua kuiacha kabisa.”


Nukuu ya mshiriki mwingine inasema “Ugumu ni mkubwa sana tunapotekeleza majukumu yetu, hasa tunapoihusisha serikali. Hii ni mwaka wa tatu au wa nne mfululizo tunazungumzia jambo lilelile. Kama serikali inashindwa kutoa ushirikiano kwa ajili ya wananchi, basi wanakuwa wameshindwa kutimiza wajibu wao kama viongozi.”

Mkutano wa Mwaka wa Makampuni ya Vyombo vya Habari ukihudhuriwa na Mkurugenzi wa JAB, Kipangula.Picha: Tanzania Journalist Accreditation Board, JAB

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameelekeza mamlaka za serikali kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pale wanapohitajika kwa mahojiano au taarifa.
Zaidi anasema “Azimio hili linapaswa kuanza kutekelezwa kuanzia leo. Nisaidieni kuniambia wizara au taasisi yoyote ambayo ikitafutwa kwa taarifa inazungusha waandishi wa habari nitakula nao sahani moja. Kama kuna mtu anapiga simu na anazungushwa, hao ni halali yangu.”

Umoja wa Mataifa:  Uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa ni haki za msingi

Kwa upande wake, Umoja wa Mataifa umeendelea kusisitiza kuwa uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa ni haki za msingi za binadamu. Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini Tanzania, Susan Manondo, anasema taarifa sahihi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Zaidi Bi Manondo anasema “Kwa Tanzania, katika hatua za kuelekea dira ya maendeleo ya 2050, taarifa sahihi zitakuwa muhimu katika kujenga uelewa wa umma na kuhamasisha wananchi kushiriki kwa uwazi katika ajenda ya mabadiliko ya taifa.”
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka huu inasisitiza umuhimu wa kuunda mustakabali wa amani, kukuza uhuru wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya haki za binadamu, na usalama wa wanahabari.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW