Mstyslav Chernov na Evgeniy Maloletka watunikiwa na DW
21 Juni 2022Waandishi habari wawili waliokusanya matukio ya kutisha katika mji wa Mariupol wametunukiwa tuzo ya DW ya uhuru wa kujieleza kutokana na kazi yao hiyo waliyoifanya wakati mji huo ukiwa umezingirwa na wanajeshi wa Urusi.
Waandishi habari hao raia wa Ukraine Mstyslav Chernov na Evgeniy Maloletka ndio walioshinda tuzo ya mwaka huu ya DW ya uhuru wa kuzungumza,na wametunukiwa tuzo hiyo kutokana na kazi kubwa waliyoifanya ya kukusanya matukio yaliyoshuhudiwa katika mji wa Mariupol licha ya mji huo kuwa chini ya mzingiro wa wanajeshi wa Urusi.Chernov anafafanua ni kwanini hivi sasa wanataka kurejea tena katika eneo la mapmbano.
Katika simulizi yake anasema katika matukio yote waliyoyaona kwenye mji huo wa Mariupol,kuna tukio moja ambalo bado limebakia kwenye kumbukumbu yake na anaiona sura ya tukio hilo kila wakati,ambalo ni mwili wa mtoto mchanga uliokuwa umelala kwenye sakafu ya hospitali moja''
Akizungumza na DW Mstyslav Chernov anasema ni hapo ndipo alipopiga picha ya mwisho katika mji wa Mariupol na kuondoka katikatika ya mwezi Marchi.Anasema walikuwa wakichukua picha na video za matukio katika hospitali ambapo daktari alimfuata na kumwambia aongozane nae uwani,na huko anasimulia,ghafla aliona miili chungunzima ikiwa imelala chini ikiwa kwenye mifuko au mengine ikiwa imefungwa na mazulia.
Simulizi ya matukio ya kutisha Mariupol
Maiti zote hizo Chernov anasema zilikuwa ni raia waliouwawa katika mashambulizi ya mabomu.Na kisha daktari huyo akampeleka chini ya jengo hilo la hospitali ambako nako alikutana na miili mingine zaidi imelezwa chini na miongoni mwao ulikuweko mwili wa mtoto huyo mchanga uliokuwa umefungwa kwenye mfuko na daktari akaufungua.Kando ya mwili wa kichanga huyo kilikuweko kipande cha karatasi kilichoandikwa ujumbe uliosema kilikuwa ni kichanga kilichokuwa na umri wa siku 23.
Chernov ni mwandishi habari mpiga picha wa shirika la habari Associated Press,yeye pamoja na mwenzake wa muda mrefu ambaye ni mwandishi mpiga picha wa rejareja Evgeniy Maloletka, wametunukiwa tuzo ya Uhuru wa kujieleza inayotolewa na DW kutokana na juhudi zao na kazi waliyoifanya ya kuripoti kilichoendelea katika mji wa Mariupol mnamo mwezi wa Februari na March.
Waandishi hao wawili waliwasili katika bandari ya mji huo saa chache kabla ya wanajeshi wa Urusi kuingia Ukraine na walianza mara moja kuripoti kutokea mji hup kwa kipindi cha wiki tatu kabla ya kuondolewa kwenye mji huo uliokuwa umezingirwa mnamo katikati ya mwezi March.Picha na video walizopiga za matukio zilikuwa zikionesha kwa kina hali ya kuogofya za mji huo uliowahi mwanzo kuwa mji wenye maendeleo,na ambao sasa umebaki kuonekana ukiwa umeporomoka na kukabiliwa na mashambulizi makubwa ya anga ya wanajeshi wa Urusi.
Kadhalika waandishi hao walichukua matukio yalionesha namna ambavyo watu walikuwa wakiishi katika hali ya kutojua la kufanya,wakiwa wamekatiwa huduma ya gesi na umeme,bila ya chakula,na maji ya kunywa kwa kipindi cha wiki kadhaa.Walirekodi pia makaburi ya watu wengi waliozikwa kwa pamoja ya raia na watoto.
Waandishi hao pia wanasema walikuwa wakiyafanya yote hayo bila ya kuwa na nafasi ya kufanya hivyo,wakati pia wakiwa hawana mtandao au wakipata matatizo makubwa ya kupata huduma hizo au kufuatilia vyombo vya habari na kuona nini watu wanachokizungumza kuhusu matukio waliyochukua video au kuyapiga picha.
https://www.dw.com/en/dw-honors-journalists-who-documented-horrors-of-mariupol-siege/a-62133022