Ripoti ya 2008
12 Februari 2008
Kiongozi wa shirika hilo la waandishi wasio na mipaka lenye makao yake mjini Paris Ufaransa Robert Menard shirika ambalo hujulikana pia kwa kifaransa kama Reporters Sans Frontiers (RSF) amesema kwamba alisema kutowajibika kwa baadhi ya magharibi na mashirika makubwa duniani ndiko kunakouhujumu na kuuathiri uhuru wa vyombo vya habari . Akaongeza katika taarifa yake kwamba ukosefu wa moyo thabiti wa nchi za kidemokrasi, katika kutetea maadili ambayo wanapaswa kuyasimamia ni jambo linalotisha.
Bw Menard hasa alililenga baraza la haki za binaadamu la umoja wa mataifa lenye makao yake makuu mjini Geneva Uswisi, ambalo amedai lisalimu amri mbele ya mbinyo kutoka nchi kama Iran na Uzbekistan, wakati huo huo akikosoa udhaifu wa umoja wa ulaya kuelekea madikteta ambao hawakushtushwa hata na kitisho cha vikwazo kutoka nchi za Ulaya.
Ripoti ya shirika hilo la waandishi wasio na mipaka kwa mwaka huu wa 2008 pia inatanabahisha juu ya kitisho kinacho wakabili waandishi habari kuanzia katika suala la usalama wao katika maeneo ya mizozo pamoja na uchujaji wa habari na vyombo vya habari kwa jumla hasa panapohusika na matatizo yanayohusiana na uchaguzi katika nchi mbali mbali mwaka huu.
Aidha imezingatia pia uchunuguzi juu ya uhuru wa vyombo vya habari katika kila kanda duniani kwa mwaka 2007 na pia kurasa za maelezo ya hali katika nchi 98.
Inataja kwamba uwezekano wa waandishi kushambuliwa wakati wa chaguzi zijazo huko Pakistan, Urusi, Iran na Zimbabwe ni mkubwa na kuna hofu kubwa ya kuandamwa katika mwaka huu 2008.
Suala jengine linalozingatiwa katika ripoti ya shirika hilo la waandishi wasio na mipaka ni wasi wasi juu ya usalama wa waandishi wanaoripoti juu ya mizozo katika nchi kama Somalia na Sri Lanka hadi Irak na maeneo ya Wapalestina.
Kuchujwa kwa vyombo vipya vya habari ni kitisho kingine kinachozingatiwa ikitajwa China ikiwa ni hatua zinazochukuliwa kabla ya michezo ya Olimpik ya majira ya joto itakayofanyika Beijing mwaka huu.
Ripoti imesema hakuna shirika lolote mbali na kamati ya olimpik ya kimataifa linaloamini kwamba serikali ya China itapiga hatua ya maendeleo fulani ya maana kabla ya michezo hiyo kuanza,kwani kila anapoachiwa huru mwandishi mmoja mwengine huingia gerezani.