1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi: Uchaguzi Kenya ulikuwa huru

10 Agosti 2017

Makundi ya waangalizi wa kimataifa yameelezea mchakato wa uchaguzi Kenya ulikuwa huru, wazi na wa haki. Makundi hayo yamesema kuwa uchaguzi huo ulifanywa katika mazingira ya amani na utulivu kote nchini.

Kenia Wahlen Thabo Mbeki und John Kerry Wahlbeobachter
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Hata hivyo kauli zao zinajiri wakati ambapo matokeo ya urais wa uchaguzi huo yanaibua utata huku upande wa upinzani unaoongozwa na Raila Odinga ukidai kuwa mitambo ya tume ya kusimamia uchaguzi ilidukuliwa, madai ambayo tume ya kusimamia uchaguzi imeyakanusha. Matamshi ya makundi ya waangalizi hawa wa uchaguzi yanatia gundi matokeo ambayo tume ya uchaguzi IEBC, imekuwa ikipeperusha kwenye mtandao wake, yakimweka mbele rais Uhuru Kenyatta wa kura milioni 8 dhidi ya kiongozi wa muungano wa NASA Raila Odinga aliye na kura milioni 6.6.

Kwenye kikao na wanahabari waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesema kuwa japo kulikuwa na changamoto kadha wa kadha kama vile kuchelewa kufika kwa vifaa vya kupiga kura katika baadhi ya vituo, utaratibu wa uchaguzi ulikuwa sawa. Wamesema kuwa asasi zilizohusika zilizingiatia uwazi kabla na baada ya uchaguzi mkuu, hivyo kuzingatia demokrasia. Ujumbe huo umesema kuwa baadhi ya mawakala wao kwenye vituo vya kupigia kura waliona mchakato huo ukianza na kukamilika. Wamepongeza wadau wote na wakenya kwa kudumisha amani katika uchaguzi huu uliokamilika siku ya Jumanne. Adan Kizimba ni mmoja wa waangalizi wa jumuiya ya Afrika Mashariki: “Uchaguzi katika vituo ulikuwa ni mzuri na ulikwenda vizuri sana vifaa vilikuja kwa wakati. Kwa sababu hiyo wananchi wa Kenya watunze usalama na amani ya wakenya.”

Matokeo kamili yasubiriwa

Wakenya waaswa kulinda amani na kuwa wavumilivu Picha: picture-alliance/dpa/AP/B. Inganga

Matamshi kama hayo yakitolewa na kiongozi wa kikundi cha waangalizi kutoka Umoja wa Afrika aliyekuwa pia rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki. Kikundi hicho kikisema kuwa jukumu la waangalizi sio kuchunguza uchaguzi ila ni kuangalia utaratibu wake. Kuhusu madai ya udukuaji wa mitambo ya tume ya kusimamia uchaguzi yaliyoibuliwa na kinara wa muungano mkuu wa upinzani Raila Odinga, Kikundi hicho kimesema kuwa, tume ya IEBC ndio yenye jibu hilo. “Sisi si wachunguzi wa Umoja wa Afrika, sisi ni waangalizi wa uchaguzi kama tu waangalizi wengine”

Aidha kikundi cha waangalizi kutoka jumuiya ya madola kimeungana na waangalizi wengine na kukariri matamshi yayo hayo. Kikundi hicho kimesema kuwa maafisa wake walizunguka katika taifa la Kenya kabla na baada ya uchaguzi na kuridhika na maandalizi yote. Kikundi hiki kiliongozwa na aliyekuwa rais wa Ghana John Dramani Mahama. “Ni matarajio yangu kuwa, mazingira ya amani tuliyoshuhudia tarehe nane Agosti yataendelea kushamiri tunaposubiri kukamilika kwa mchakato huu wa uchaguzi.”

Makundi mengine ambayo yametoa kauli zao ni pamoja na Kikundi cha waangalizi kutoka marekani kikiongozwa na aliyekuwa waziri wa masuala ya mambo ya nje wa marekani John Kerry kilichosema kuwa kuwa wakenya wengi walijitokeza kutekeleza haki yao ya kidemokrasia. Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa wanashikilia kuwa jukumu la waangalizi linastahili kupita mipaka ya kuangalia tu mchakato wa uchaguzi na kufikia kiwango cha kuchunguza. Ripoti kamili za waangalizi hawa zitatolewa baada ya miezi miwili. Je, ripoti hizo zitakuwa na maana kwa matokeo ambayo yatakuwa yametangazwa na kuamuliwa?

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW